Ziara ya rais Ruto kwa ndege ya kigeni yaendelea kuzua mjadala

Ziara ya rais Ruto kwa ndege ya kigeni yaendelea kuzua mjadala

Rais amesema kuwa kusafiri na ndege ya taifa ya Kenya Airways ingekuwa bei ghali zaidi.
Kenya's President William Ruto arrived in the US on Monday. Photo / State House

Ziara ya rais William Ruto Marekani inaendelea kuzua mjadala nchini Kenya hasa baada ya rais Ruto kuteteta matumizi yake ya ndege ambayo ilikuwa ya kigeni na wala si ndege ya taifa ya Kenya Airways.

Ripoti nchini Kenya zilisema kuwa serikali ilitumia shilingi milioni 200 (dola milioni 1.5) kukodi ndege hiyo binafsi kutoka kwa kampuni ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Ilikuwa ndege aina ya Boeing 737-700.

"Wakenya wenzangu, nimeona wasiwasi kuhusu njia yangu ya usafiri hadi Marekani. Kama Kiongozi anayewajibika kwa rasilimali za umma na kulingana na azimio langu kwetu kuishi kulingana na uwezo wetu na kwamba ninapaswa kuongoza kutoka mbele kwa kufanya hivyo, gharama ilikuwa ndogo kuliko kusafiri kwa KQ," Rais Ruto alisema katika akaunti yake ya X.

Hata hivyo Wakenya wameichukulia hiyo kwa njia tofauti.

"Mkenya mwenzetu. Kudai kuwa tunajenga upya uchumi wetu. Pia, "Pan-Africanist" lakini imelipa US$1.5M kukodi ndege binafsi kutoka nchi ya kigeni. Sio hata Afrika. KQ inamilikiwa kwa sehemu na serikali ya Kenya. Kila mara unahitaji uokoaji wa kifedha ... lakini HAPANA, unakomboa kutoka UAE! Mwenye hekima!." mwananchi mmoja alimjibu rais.

Ndege ya taifa ya Kenya Airways ilianzishwa mwaka wa 1977/ Picha: Reuters 

"Afadhali utumie milioni 300 katika KQ kuliko kukodisha ndege binafsi kutoka nchi nyengine ambapo ni vipaumbele vyako," mwananchi mwingine akaongezea.

"Ili kuepuka dhana potofu zaidi, tupe takriban kiasi ulichotumia na zile ambazo KQ ingeweza kutoza," mwingine alisema.

"Kama rais, ni jukumu lako kukuza yetu, lakini kwa bahati mbaya, unaua tasnia ya ndani! Ushuru wetu unaendelea kuinusuru KQ ambayo hata mkuu wetu wa nchi hawezi kuitumia, ni chukizo," mwananchi alimjibu rais.

Hata hivyo wengine walikubaliana naye.

"Hili ni wazo zuri sana. Asante kwa kutumia usafiri wa bei nafuu," Mkenya mmoja alimwambia rais.

"Lazima kuna ukweli fulani," mwingine alijibu.

Ndege ya Taifa

Kenya ina ndege ya taifa.

Kampuni ya Kenya Airways Ltd. inayojulikana zaidi kama Kenya Airways, au KQ ni shirika la ndege linalobeba bendera la Kenya. Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1977, baada ya kuvunjwa kwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki.

Shirika hilo la ndege lilikuwa linamilikiwa na Serikali ya Kenya hadi Aprili 1995, na lilibinafsishwa mwaka wa 1996.

Kenya Airways kwa sasa ni ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.

Serikali ya Kenya ina hisa kubwa 48.9%, huku 38.1% ikimilikiwa na kampuni inayoitwa KQ Lenders Company 2017 Ltd. Hii inamilikiwa na muungano wa benki.

Kampuni ya ndege ya KLM yenye asili ya Waholanzi ina hisa 7.8% katika kampuni hiyo.

Hisa zilizosalia zinamilikiwa na wamiliki binafsi huku hisa zake zinauzwa kwenye Soko la Hisa la Nairobi, Soko la Hisa la Dar es Salaam, na Soko la Dhamana la Uganda.

Ndege ya rais, Harambee One

Kenya ina ndege ya rais.

Ndege ya rais, maarufu kama Harambee One, ni ndege ya masafa marefu ya Fokker 70. Ililetwa nchini mnamo Disemba 1995.

Ilinunuliwa na serikali ya rais wa wakati huo ya Daniel Arap Moi.

Mwezi Aprili 2024, wabunge kadhaa walipeleka muswada bungeni wakitaka bunge iidhinishe ununuzi wa ndege mpya ya rais . Walidai kuwa ndege ya sasa ya rais ni kuukuu na haiwezi kwenda masafa marefu.

Wengine walisema inafaa kubadilishwa kuhakikisha usalama wa rais na hata wanajeshi wa anga ambao wana jukumu ya kuiendesha.

TRT Afrika