Netanyahu / Picha: AFP

Na Sylvia Chebet

"Afadhali kuchelewa kuliko kutowasili kabisa."

Wakati mwanasheria wa haki Francis Boyle alipotamka maneno hayo akijibu ombi la mwendesha mashtaka Karim Khan wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutafuta hati za kukamatwa dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, waziri wa ulinzi Yoav Gallant kwa madai ya uhalifu wa kivita, huenda alikuwa akitoa sauti ya hisia za kila mtu aliyepoozwa na vitendo vya kutisha vya Gaza.

Picha za kusikitisha za watoto waliojeruhiwa na kufa, wazazi waliolia wakichimba vifusi kwa mikono yao kwa matumaini ya kuokoa maisha, na mateka walioko maeneo yasiyojulikana, hatima yao haijulikani — Gaza imekuwa jehanamu duniani kwa miezi minane sasa.

Kila alfajiri ni mualiko mpya wa kifo na uharibifu zaidi, shinikizo lilikuwa linaongezeka kwa ICC kuchukua hatua.

"Unangoja nini, Bwana Khan?" balozi wa Libya UN, Taher El-Sonni, alimuuliza mwendesha mashtaka wa ICC. "Hauoni vitisho kwa raia? Dunia inatarajia ICC kuwa na ujasiri na kutoa hati za kukamatwa dhidi ya maafisa wa utawala wa Israeli," alisema.

Khan alisema alikuwa na sababu za kutosha kuamini kwamba Netanyahu, Gallant na viongozi watatu wa Hamas wanawajibika kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 2023.

Shambulio la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, ambapo watu 1,200 waliuawa, limetumiwa na utawala wa Netanyahu kama kisingizio cha mashambulizi ya risasi, mabomu na makombora ambayo yamekuwa yakimiminika Gaza tangu Oktoba 8 mwaka jana hadi leo.

Khan alisema Israel ilishindwa kutii sheria za kimataifa za kibinadamu.

"Njia ambazo Israel ilichagua kufikia lengo lake Gaza – yaani, kusababisha kifo, njaa, mateso makubwa, na majeraha makubwa kwa mwili au afya ya raia – ni za jinai," mwendesha mashtaka alisisitiza.

Boyle, ambaye alimshawishi Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kukubali mamlaka ya ICC, alisema kwamba uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu umetendeka nchini Palestina tangu Nakba ya mwaka 1948.

"Kwa miaka 15, licha ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, waendesha mashtaka watatu huru tofauti hawakufanya lolote kuwasaidia Wapalestina hadi leo. Kwa hiyo, ahsante Mungu," aliiambia TRT Afrika.

Nini kinachofuata?

ICC

Ombi la mwendesha mashtaka wa ICC linapelekwa kwa majaji watatu kutoka Romania, Mexico na Benin ambao wataamua ikiwa masharti ya kutoa hati za kukamatwa yametimizwa.

Hata hivyo, majaji hawana muda maalum wa kuamua ni lini watatoa hati za kukamatwa zilizopendekezwa. Katika hafla za awali, majaji wamejulikana kutumia muda ya zaidi ya mwezi mmoja hadi miezi kadhaa kutoa maamuzi kuhusu maombi kama hayo.

"Kuhusu ombi lake la hati za kukamatwa dhidi ya Rais Vladimir Putin (wa Urusi) na watu wake huko, naamini walipata hiyo ndani ya wiki nne," Boyle alikumbuka.

Profesa wa sheria katika Chuo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Illinois nchini Marekani anaamini kwamba siasa za kimataifa zinaweza kuathiri uamuzi wa paneli. "Nina uhakika Marekani, Israel na Wazayuni wataweka shinikizo kubwa kwa majaji hawa wa ICC. Kwa hiyo, tutalazimika kuona nini kitatokea hapa."

Tayari, wabunge wawili wa Republican nchini Marekani wameanzisha "Sheria ya Kupinga Mahakama Isiyo Halali" kuweka vikwazo kwa maafisa wa ICC wanaofuatilia nchi hiyo au washirika wake, ikiwa ni pamoja na Israel.

Iwapo ICC itatoa vibali vya kukamatwa kwa viongozi wa Israel na Hamas, ulimwengu wao ungekuwa mdogo lakini bado wanaweza kusafiri katika mataifa rafiki. / Picha: AA

"Nasisitiza kwamba majaribio yote ya kuzuia, kutisha au kushawishi vibaya maafisa wa mahakama lazima yasitishwe mara moja," mwendesha mashtaka wa ICC Khan alisisitiza katika uamuzi wake wa Mei 20.

Majaji wakikubali kwamba kuna "sababu za msingi" kuamini kwamba uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinadamu umetendeka, wata toa hati za kukamatwa.

Vikwazo vya kusafiri

Swali kubwa linalofuata ni: Je, Netanyahu, Gallant na viongozi wa Hamas watakamatwa?

Mkataba wa Roma, ambao ulianzisha mahakama hiyo, unalazimisha nchi zote 124 wanachama wa ICC kukamata na kuwasilisha mtu yeyote — anayekabiliwa na hati ya kukamatwa ya ICC — endapo ataingia katika eneo lao.

ICC haina kikosi cha polisi cha kukamata watuhumiwa. Badala yake, mkataba unaoanzisha mahakama hiyo unalazimisha nchi wanachama kukamata watuhumiwa na kuwakabidhi kwa ICC kila wanapoingia katika eneo lao. Hata hivyo, mataifa kadhaa yamepuuza jukumu hili na kupokea adhabu zaidi.

Mahakama ikikubali maombi ya mwendesha mashtaka wa ICC, viongozi wa Israeli na Hamas watajiunga kinadharia na orodha ndefu ya watuhumiwa wa uhalifu wa kivita ambao bado wako huru.

"Watakua wakimbizi kwa maisha yao yote," alisema Boyle, akionyesha kwamba mashtaka hayazuii uhuru wao wa kusafiri.

"ICC haina mamlaka kwa Israel iliyofafanuliwa na mipaka ya 1967 kwa hiyo, Netanyahu na wengine watakaa huko maisha yao yote."

Hata hivyo, uongozi wa Israeli unafurahia msaada wa Washington na unaweza kusafiri kwa usalama kwenda na kutoka nchi hiyo. "Lakini ni hivyo tu," alisema Boyle.

Orodha ya wanaosakwa zaidi

Ilianzishwa mnamo 2002, majaji wa ICC tangu wakati huo wametoa hati 46 za kukamatwa. Kulingana na tovuti ya Mahakama, watu 21 wamezuiliwa katika kituo cha kizuizini cha ICC huko The Hague, Uholanzi, kutokana na ushirikiano wa Nchi, na wamefika mbele ya Mahakama.

Watu 17 bado wako huru. Mashtaka yametupiliwa mbali dhidi ya watu 7 kutokana na vifo vyao.

Majina maarufu kwenye orodha ya waliowahi kutafutwa zaidi ya ICC ni pamoja na Putin wa Urusi, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita kutokana na vita na Ukraine. Mahakama ilitoa hati ya kukamatwa dhidi ya Putin mnamo Machi 2023.

Mserbia Slobodan Milosevic alifariki katika kituo cha ICC mwaka 2006. Alikuwa mkuu wa kwanza wa nchi kushtakiwa kwa mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Picha: Reuters

Omar al-Bashir wa Sudan anashtakiwa kwa kupanga mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita katika eneo la Darfur la Sudan, ambapo watu takriban 300,000 waliuawa. Hati ya kukamatwa kwake ilitolewa mnamo 2009 alipokuwa rais. Ingawa al-Bashir baadaye alipinduliwa na kukamatwa, hakukabidhiwa kwa The Hague.

Mhalifu wa kivita wa Uganda Joseph Kony, kiongozi wa Jeshi la Upinzani (LRA) anayetuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ndiye mkimbizi wa muda mrefu zaidi wa ICC.

Hati ya kukamatwa kwake ilitolewa mnamo 2005. Mapema mwaka huu, majaji waliruhusu waendesha mashtaka kuleta kesi dhidi yake akiwa hayupo.

Licha ya safari ngumu, Boyle, ambaye alihusika na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Yugoslavia (ICTY), anaamini bado inawezekana kupata haki.

"Gurudumu la haki za kimataifa ni linasogea polepole, lakini linatembea," alisema.

"Nilifungua mashatka juu ya Slobodan Milosevic na ICC mnamo Machi 1993. Nilimfuata kwa ajili ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu dhidi ya Wabosnia. Kisha nilimshawishi mwendesha mashtaka wa ICTY, Carla Del Ponte, kumshtaki Milosevic kwa karibu kila uhalifu katika sheria, ikiwa ni pamoja na makosa mawili ya mauaji ya kimbari."

Kiongozi huyo mzee wa Serbia hatimaye alifunguliwa mashtaka huko The Hague mnamo 2004.

Boyle alitembea kwenye maeneo ya mauaji ya Srebrenica mashariki mwa Bosnia na Herzegovina, ambapo karibu watu 8,000 waliuawa. Anaona hali huko Gaza kuwa sawa na mauaji ya kimbari ya 1995.

"Wapalestina 40,000 wameangamizwa. Themanini elfu wamejeruhiwa, na Gaza yote imeharibiwa kabisa... Kwa hiyo kama hawakuchukua hatua, wangeingia katika jalala la historia."

Maswali kuhusu kuwalenga Waafrika

Kiongozi wa wanamgambo wa Lords Resistance Army, LRA, Joseph Koni | Picha: AFP

Hii ni mara ya kwanza ICC inamfuata kiongozi wa Magharibi.

"ICC inaitwa mahakama ya mtu mzungu," alisema Boyle.

Kufikia wakati mwendesha mashtaka wa kwanza, Luis Moreno Ocampo, alipoondoka ofisini mnamo 2012, ICC ilikuwa na uchunguzi sita wazi — zote Afrika – ikivutia ukosoaji kwamba ilikuwa kimsingi ni mahakama ya Ulaya iliyoundwa kuwashtaki Waafrika.

Ombi la hati za kukamatwa dhidi ya Netanyahu wa Israeli na Gallant huenda linavunja mpangilio huo.

"Leo, tunasisitiza tena kwamba sheria za kimataifa na sheria za migogoro ya kivita zinatumika kwa wote. Hakuna askari, hakuna kamanda, hakuna kiongozi wa kiraia – hakuna mtu – anayeweza kutenda bila adhabu," alisema Mwendesha Mashtaka Khan.

Boyle anaamini kwamba "ni hali ngumu sana kuzuia mauaji ya kimbari yanapokuwa yanaendelea". Lakini ana matumaini kwamba mashtaka yanaweza kuwafanya wanajeshi wa Israeli kufikiria upya maamuzi yao na labda kuchangia kusitisha mapigano mara moja na kwa kudumu huko Gaza.

Zaidi ya Mashariki ya Kati, wengine sasa wanataka washirika wa Israel, hasa wale wanaoipa silaha, kuwajibishwa.

TRT Afrika