Wagner Fighters/ Photo AA

By Awa Cheikh Faye

Wagner inatuhumiwa kuendesha operesheni haramu, kukiuka haki za binadamu na kuvuruga utulivu wa nchi za Afrika. Kwa hivyo, Wagner inafanya nini katika eneo la Afrika lenye ushawishi wa Ufaransa jambo ambalo lina athari nyingi za kisiasa, kiuchumi na usalama?

Mshirika mpya dhidi ya makundi yenye silaha

Jamhuri ya Afrika ya Kati, taifa lisilozungukwa na bahari, likiwa katikati mwa bara hilo, iko katika lindi la mzozo mkubwa wa usalama.

"Hii inahusu sana usalama wa ndani, mzozo wa kijamii ambao mamlaka haiwezi tena kuudhibiti. Jeshi la Afrika ya Kati halina tena njia ya kukabiliana na mzozo huu.

Hii ndiyo sababu Jamhuri ya Afrika ya Kati iliomba msaada wa silaha kwanza kutoka kwa washirika wake wa jadi yake kwa ajili ya FACA (Jeshi la Afrika ya Kati)," Hassane Koné wa Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS Africa) anaiambia TRT Afrika.

"Msaada haukufika. Hivyo kutokana na nia ya kubadilisha ushirikiano, CAR (Jamhuri ya Afrika ya Kati) ikawafikia Warusi," anaelezea.

Tangu mwaka 2013, Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa chini ya vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Hii ni pamoja na kupiga marufuku uwasilishaji wa silaha, risasi, magari ya kijeshi na vifaa. "Kuwepo kwa Wagner katika eneo hilo kulisadifiana na kipindi cha kupungua kwa ushawishi wa Ufaransa katika kanda hiyo, iliyoakisiwa na matokeo mseto katika masuala ya operesheni za kijeshi barani humo.

Kutokana na hali hiyo, wakazi wa eneo hilo, hasa vijana, walipoteza imani kwa Ufaransa," anasema Dk Moumouny Camara, mhadhiri na mtafiti katika sayansi ya habari na mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop huko Dakar.

Koné, mtaalam wa masuala ya usalama, anashawishika kwamba mshirika wa jadi wa bara hilo, Ufaransa, "haijajibu changamoto za usalama zinazokabili nchi za Afrika".

Madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu

Wakati wanamgambo wa Wagner Group wakiendelea na jukumu muhimu katika kutoa mafunzo kwa FACA na kuratibu shughuli zao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamejitenga na vikosi vya Serikali katika angalau 50% ya matukio yanayohusiana na vurugu za kisiasa tangu Mei 2021 - isipokuwa kuanzia Oktoba mwaka huo mpaka Aprili na Juni 2022.

Maelezo haya yanakusanywa na Mradi wa Data ya Eneo na Tukio la Migogoro (ACLED), shirika linalokusanya na kuchambua data na ramani huria.

Anicet Kyancem, mwanachama wa jumuiya ya kiraia ya Afrika ya Kati, anaiambia TRT Afrika kwamba "askari wa Ufaransa waliohusika katika operesheni ya Sangaris pia walitajwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji wa kingono kwa watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2014".

Baada ya kurudi katoka ziara ya siku 10 nchini Mali, Alioune Tine, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, amewashutumu wanamgambo wa Wagner kwa "kuwatia hofu" wakazi wa eneo hilo.

Katika ripoti iliyochapishwa kwenye tovuti yake, ACLED ilirekodi "karibu vifo 480 vya raia vilivyohusishwa na operesheni zilizofanywa na wanamgambo wa Wagner na pamoja na vikosi vya Mali".

Ingawa Serikali ya Mali haijawahi kukiri rasmi uhusiano wowote au ushirikiano na kundi la Wagner, ripoti kadhaa za uchunguzi zinaonyesha kuhusika kwa kundi hili katika ukiukaji wa haki za raia nchini Mali.

Bamako amekataa madai haya moja kwa moja na kukana ushirikiano wowote na Kundi la Wagner.

Harakati za Kidiplomasia na kiuchumi

Kundi la Wagner limekuwa likifanya kazi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu 2018, kufuatia kusainiwa kwa makubaliano kati ya nchi hiyo na Serikali ya Urusi. Lakini Urusi, mara nyingi, imekataa uhusiano wowote na kikundi hiki.

Dk Moumouny Camara anaamini kuwa iwe rasmi au si rasmi, madai ya ushirikiano kati ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Urusi yanaashiria mafanikio ya kidiplomasia kwa Urusi.

"Imekuwa njia ya kufungua soko la Afrika kwa makampuni ya Urusi," anasema. Hakika, Moscow haijaficha azma yake ya "kuteka tena" soko la Afrika.

Mnamo mwaka wa 2019, mkutano wa kilele wa Afrika na Urusi ulimkutanisha Rais wa Urusi Vladimir Putin na viongozi zaidi ya 40 wa Afrika kujadili ushirikiano, haswa katika masuala ya biashara.

Ingawa uhusiano wa kibiashara kati ya Urusi na Afrika bado ni dhaifu, Moscow inawekeza zaidi kuliko hapo awali katika nyanja za usalama na kisiasa.

Huko Bangui, hakuna siri kwamba uungwaji mkono wa Kundi la Wagner katika vita dhidi ya makundi yenye silaha una gharama.

"Lazima mkumbuke kwamba nchi hii imejaa maliasili ambazo zinaweza kuwavutia Warusi. Tuna dhahabu kila mahali, na Wagner Group wapo maeneo ambapo kuna vikundi vyenye silaha vinavyo nyonya maliasili za nchi, hasa dhahabu na almasi. Kile tunachopaswa kutoa kwa ajili ya usalama wa nchi, basi tunaweza kufanya hivyo”, anasema Kyancem.

Suala la mtazamo

Uvumi wa kuwepo kwa kundi hilo la kijeshi nchini Burkina Faso ulikuwa umeenea kwa muda kabla ya kukanushwa vikali.

Ouagadougou imeweka wazi kuwa haishirikiani na mtu yeyote. Burkina Faso inataka kupambana na ugaidi katika eneo lake peke yake huku ikiwa haiondoi uwezekano wa kutafuta "njia" ya jawabu la kupambana na ugaidi kutoka kwa washirika mbalimbali.

Kwa mtazamo wa Kyancem, usalama wa watu na uhuru wao wa kufanya biashara zao una umuhimu mkubwa kuliko jambo lingine lolote.

"Kama raia wa kawaida, nataka kuzunguka, kwenda kijijini kwangu na kuona watu vijijini. Nchi yetu ni maskini, lakini tunahitaji uhuru wa kutembea. Ikiwa kikundi cha [Wagner] kinaweza kutoa usalama safarini, na iwe hivyo. . Hili ndilo jambo pekee la maana" anaiambia TRT Afrika.

Mtaalamu wa usalama Koné anaamini kuwa upatikanaji wa silaha bora hivi karibuni umeathiri uhusiano kati ya nchi za Afrika na washirika wao wa jadi.

"Washiŕika wapya wa Afŕika kama vile Russia, Uchina, Uturuki na Bŕazili wanauza silaha kwa nchi zetu na kuziwasilisha kwa urahisi zaidi, kwa bei nafuu, na bila vikwazo vyovyote vilivyowekwa na mataifa ya Maghaŕibi,” anaelezea.

Koné anapendekeza kuimarisha na kuunganisha majeshi ya kitaifa kwa kuwekeza katika vifaa na kutoa mafunzo kwa vikosi vya ulinzi na usalama vya taifa badala ya kutegemea watu wa nje kufanya kazi hii muhimu.

"Usalama wa kuazima kutoka nje si endelevu. Utumiaji wa wanamgambo unazidisha hali ya ukosefu wa utulivu, ghasia na machafuko," anasema.

Pia anasisitiza umuhimu wa kuchanganya mbinu ya usalama na mkakati madhubuti wa kisiasa na kijamii na kiuchumi ili kuondokana na itikadi hatarishi, uhalifu uliopangwa na machafuko ya kijamii ambayo yanachochea ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.

TRT Afrika