Na Susan Mwongeli
Kwa miongo kadhaa, Waafrika wa Magharibi wamekuwa wakijadili kuhusu nani anatengeneza wali wa jollof nzuri na bora zaidi. Nigeria, Ghana, Senegal, Cameroon, na Gambia wote wanadai kuwa na mapishi bora zaidi ya wali wa jollof.
Na ni hivyo pia kwa nchi za Sierra Leone, Cameroon, Togo, Côte d'Ivoire, Liberia, na Mali.
Mwaka 2023, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilitambua Senegal kama chimbuko la ladha hii ya kipekee ya mapishi.
Kulingana na UN, jolloff kutoka Senegal ni hazina kwa watu wa Senegal.
Licha ya tangazo hili, nchi nyingine za kanda ya Afrika Magharibi, hasa Nigeria na Ghana, zinaendelea kutofautiana kuhusu nani anatengeneza aina nzuri zaidi ya wali wa jollof.
Wali wa jollof ni nini?
Ni chakula kinachotengenezwa kwa kutumia sufuria moja na inajumuisha mchele, mafuta, nyanya, paste ya nyanya, vitunguu na viungo vingine.
Haya ni msingi tu, kwani kuna viungo vingi vingine vinavyotumika, kulingana na utamaduni wa asili wa mtu.
Basi, kwanini jollof inaleta mjadala mkubwa? Kweli, ni zaidi ya chakula tu kwa wale wanaoipenda.
Inawakilisha mshikamano, furaha, na urithi wa kitamaduni. Mara nyingi huliwa kwenye harusi, sherehe za siku ya kuzaliwa, na tamasha za kitamaduni.
Mjadala kuhusu nchi yenye sahani bora zaidi ya jollof daima huendelea kwenye mitandao ya kijamii na inaonekana kama haijawahi kupatika ufumbuzi. Mara nyingi ni moto zaidi kati ya Wanigeria na Waghana.
''Jollof ya Ghana bila shaka ndiyo Jollof nzuri zaidi barani Afrika. Mara nyingi inatiwa viungo kwa kutumia mchuzi wa nyanya na samaki. '' Hafiz Tijani kutoka Ghana anasema akiamini kwamba nchi yake inashikilia taji la jollof bora.
''Harufu pekee kabla ya kula chakula inaacha mtu na mawazo yasiyosahaulika. Kula Jollof iliyotengenezwa Ghana haisaidii tu kuondoa njaa, bali pia inakupa raha,'' Hafiz anaiambia TRT Afrika.
Chef Racheal kutoka Nigeria, hata hivyo, ana hoja ya kupinga.
''Umaarufu wa jollof kutoka Nigeria ndio unafanya mapishi yetu kuwa ya kipekee. Hakuna nchi nyingine ya Afrika inapika Jollof kwa njia hii. Kwa kuwa mapishi yetu ya jollof yanatofautiana na ya wengine. Hii inafanya yetu kuwa bora zaidi.''
Chakula hicho, hata hivyo, inaaminika kwamba kilianzia miongoni mwa watu wa Wolof nchini Senegal na Gambia.
Wao ni kikundi kikubwa zaidi cha kikabila nchini Senegal, na wamejazana katika eneo la kaskazini mwa nchi karibu na Mto Senegal na Mto Gambia.
Wakati wa kipindi cha mwanzo cha ukoloni, watawala wa kigeni walileta mchele uliovunjika kama sehemu ya vyakula vyao vya kawaida.
Imeandikwa kwamba Wassenegal walipenda mchele zaidi kuliko nafaka. Hii ilisababisha kuundwa kwa Ceebu jën, chakula maarufu nchini humo.
Umaarufu wa chakula hicho baadaye ulisambaa hadi nchi nyingine za kanda ya Afrika Magharibi.
Biashara, uhamiaji, ndoa za mchanganyiko, na uhamisho wa kitamaduni inasemekana ilisababisha kueneza umaarufu wa chakula hicho. Na kilichojulikana leo kama wali wa jollof kilikuwa chanzo cha fahari na utambulisho wa kitamaduni kwa kanda ya Afrika Magharibi.
Kuwapikia jollof wageni inaonekana kama ishara ya ukarimu. Waghana wanaandaa wali wao wa jollof kwa kutumia mchele wenye harufu nzuri wa basmati, na mara nyingi huongeza protini kama kuku au nyama kwenye chakula.
Wanigeria wanapenda kupika na mchele wa nafaka na mafuta ya mawese, samaki, kuku au nyama. Kwa mujibu wao, mchele ukiwa kavu zaidi, ndivyo unavyokuwa na ladha bora zaidi.
Watu wa Cameroon hutumia nyama wakati wa kupika jollof yao, wakati Wasenegal huongeza mafuta ya mawese.
Kama watu wa Afrika Magharibi wengi, Waliberia pia huongeza pilipili kwenye jollof yao. Mjadala, ambao unaonekana kutokuwa na makubaliano yanayokubaliwa na wote ni nani anatengeneza jollof bora zaidi?