Xavi, mwenye umri wa miaka 44, alirejea Barcelona kuwa kocha mnamo Novemba 2021 kutoka Qatar.  / Picha: AFP

Xavi Hernandez ataendelea kuinoa Barcelona hadi 2025, Rais wa klabu hiyo Joan Laporta, amesema katika kikao na waandishi wa habari siku ya Alhamisi.

Hii ni baada ya kocha huyo kubadili uamuzi wake wa awali wa kujiuzulu mwishoni mwa msimu huu.

"Nimepata imani ya rais, benchi la ufundi na bodi nzima. Ushirikiano wa wachezaji, na mashabiki pia umekuwa muhimu sana na wamenifanya niamini mradi huu unapaswa kuendelea hata kama hatutashinda taji msimu huu. Nadhani ni uamuzi bora, " Xavi alisema.

Joan Laporta aliungana na Xavi kutoa sababu iliyowasukuma kocha na klabu hiyo kuendelea kuwa pamoja.

"Tunajua kwamba alitoa taarifa katikati ya msimu, lakini leo tuna habari njema kwamba habanduki na amenifikishia shauku na ujasiri alionao katika mradi huu," Laporta alisema.

Xavi, mwenye umri wa miaka 44, alirejea Barcelona kuwa kocha mnamo Novemba 2021 kutoka Qatar.

"Hisia ya kuwa kocha wa Barcelona ni ya kikatili, haifurahishi, unahisi kama haupati heshima unayostahili," Xavi alisema kufuatia msururu wa matokeo duni ikiwa ni pamoja na kufungwa 5-3 na Villarreal, kupoteza dhidi ya Girona, Real Madrid na Athletic Club.

Kwa sasa, ni wazi kuwa matumaini ya kutwaa ubingwa yamefifia kwa Barcelona haswa ikiwa imeachwa nyuma kwa alama 11, katika msimamo wa Ligi Kuu, kufuatia kufungwa mabao 3-2 kwenye El Clasico siku ya Jumapili.

Reuters