Erdogan

Uvamizi wa polisi wa Israel kwenye Msikiti wa Al-Aqsa huko Jerusalem Mashariki "haukubaliki," Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema Jumatano, akiitaka Israel iachane na hatua zinazo chochea mvutano.

"Uingiliaji na vitisho dhidi ya utakatifu na umuhimu wa kihistoria wa Msikiti wa Al-Aqsa pamoja na uhuru wa dini na maisha ya Wapalestina lazima ukome," Erdogan alisema katika mahojiano ya televisheni.

Matamshi yake yalikuja baada ya mvutano kuzidi ambapo polisi wa Israel waliwazuilia karibu waumini 350 kutoka ndani ya jengo la Msikiti wa Al-Aqsa.

Kundi la Wapalestina lilijizingira ndani ya Ukumbi wa Swala ya Al-Qibli katika jengo la Msikiti wa Al-Aqsa baada ya wayahudi kutoa wito wa kuvamiwa msikiti huo.

Walijaribu kuzuia polisi kuingia kwa kufunga milango yake. Wakiwa wamezunguka Jumba la Swala la Al-Qibli, polisi wa Israel walipanda juu ya paa la msikiti huo, wakavunja madirisha, na awali walitumia mabomu ya sauti dhidi ya waumini waliokuwa ndani.

Baadhi katika msikiti huo walijaribu kuwapinga polisi kwa kuwarushia fataki.

"Tutaendelea kusimama pamoja na kaka na dada zetu wa Palestina chini ya hali zote na kulinda maadili yetu matakatifu. Israel inapaswa kujua hili pia," Erdogan alisema.

TRT World