| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Madagascar yapewa Kituo cha kukabiliana na Dharura
Msaada huu unakuja wakati ambapo Madagascar inakabiliwa na hali ngumu ya mlipuko wa Mpox na athari za kimbunga
Madagascar yapewa Kituo cha kukabiliana na Dharura
Afrika CDC imeikabidhi rasmi Madagascar Kituo cha Kukabiliana na Dharura za Afya ya Umma. / Picha: Africa CDC / Public domain
tokea masaa 10

Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, Afrika CDC kimeikabidhi rasmi Madagascar Kituo cha Operesheni za Dharura ya Afya ya Umma, ikiashiria hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa kujiandaa na kukabiliana na dharura nchini humo.

"Msaada wa Afrika CDC ulijumuisha miundombinu ya kisasa na vifaa vyenye thamani ya takriban Dola za Marekani 300,000," Africa CDC imesema katika taarifa.

"Hii ni pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi 40 wa afya walio mstari wa mbele katika usimamizi wa Kituo cha Uendeshaji wa Dharura na Mfumo wa Kudhibiti Matukio," imeongeza.

Msaada huu unakuja katika wakati mgumu huku Madagascar ikikabiliana na mlipuko wa Mpox na athari za Kimbunga Fytia na Gezani.

Madagascar wakipambana na mlipuko wa Mpox

Mpox ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unaweza kusababisha upele wenye maumivu, kuvimba, homa kali, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, maumivu ya mgongo na kupungua kwa nishati mwilini.

Kulingana na Africa CDC, Madagascar inakabiliwa na mlipuko wake wa kwanza wa Mpox (aina ya clade 1b), kuanzia mwishoni mwa Disemba 2025 na kushika kasi mapema 2026.

Shirika la Afya Duniani, WHO lilisema hadi mapema Februari 2026, zaidi ya watu 250 walithibitishwa kuwa na maambukizi.

WHO ilisema mlipuko huo unahusisha watoto na umesababisha juhudi za kukabiliana na dharura.

WHO inasema kifo cha kwanza cha mtoto kiliripotiwa Machi 2, 2026.

Maeneo ambayo yameathiriwa zaidi nchini Madagascar ni Boeny na hivyo kuchochea juhudi za kitaifa za kukabiliana na hali ya dharura ya maambukizi ambayo mpaka sasa yameenea kwa kasi kwa zaidi ya mikoa 16, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Analamanga.

WHO inasema mipango inaendelea ya kutoa chanjo, ikilenga makundi yaliyo hatarini kama vile wafanyakazi wa afya na walio na mawasiliano ya karibu na wagonjwa.

CHANZO:TRT Swahili