Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kuwa nchi yake haikupokea “senti” yoyote kutoka nchi yoyote ya nje, ili kufanikisha ujenzi wa bwawa la kufua umeme, maarufu kama Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD), akipinga madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuwa Marekani iliyofadhili mradi huo.
Akihutubia bunge la nchi hiyo, Abiy alisema kuwa ujenzi wa bwawa hilo, ulitekelezwa na vyanzo vya ndani vya Ethiopia.
Bwawa hilo, ambalo limejengwa kwenye mto Nile karibu na mpaka wa Sudan, ndiyo bwawa kubwa la kufulia umeme kwa sasa barani Afrika.
Akizungumza ndani ya Ikulu ya Marekani mwishoni mwa mwezi Januari, Trump alihoji ni kwa nini serikali ya Marekani ilifadhili mradi huo, madai yaliyopingwa na Ethiopia.
Abiy aliongeza kuwa, Ethiopia inakamilisha mradi mwingine wa ufuaji umeme katika mto Omo, utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha gigawati 6,460 za umeme kwa mwaka.












