| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Waziri Mkuu wa Ethiopia ateua serikali mpya ya Tigray, ataka uchaguzi ndani ya miezi sita
Waasi wa Tigray People's Liberation Front (TPLF) waliongoza mashambulizi mwezi uliopita dhidi ya serikali ya Abiy, jambo lililochochea upya vita
Waziri Mkuu wa Ethiopia ateua serikali mpya ya Tigray, ataka uchaguzi ndani ya miezi sita
Ethiopian Prime Minister Abiy Ahmed sworn-in in Addis Ababa

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ameteua serikali ya mpito kwa ajili ya kuleta utulivu katika eneo la Tigray, kaskazini mwa nchi hiyo, na kuandaa mazingira ya uchaguzi ndani ya miezi sita. Hii inafuatia kuibuka kwa mapigano kati ya jeshi la Ethioipia na waasi.

Waasi wa Tigray People's Liberation Front (TPLF) waliongoza mashambulizi mwezi uliopita dhidi ya serikali ya Abiy, jambo lililochochea upya vita vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu kati ya mwaka 2020 na 2022.

Mzozo huo mpya umesababisha kuvunjika kwa uhusiano kati ya Ethiopia na Eritrea.

Ethiopia inaituhumu Eritrea kwa kuwasaidia waasi, tuhuma ambazo Eritrea imezikanusha.

TPLF, chama tawala cha Tigray, kilitawala siasa za Ethiopia kwa miongo kadhaa hadi pale Abiy alipoingia madarakani mwaka 2018.

Tangu mapigano yalipoanza, jeshi la Ethiopia pamoja na wanamgambo wanaounga mkono serikali wamepata mafanikio makubwa na kudhibiti maeneo mapana ya Tigray, ikiwemo mji mkuu wa eneo hilo, Mekelle.

Ofisi ya Waziri Mkuu Abiy imesema kuwa utawala huo wa mpito utadumu kwa miezi sita, kwa lengo la kuunda mazingira thabiti ya kisiasa yatakayoruhusu kufanyika kwa uchaguzi huru na wa wazi ndani ya kipindi hicho.

"Ili kupata amani ambayo imekuwa ikikosekana kwa muda mrefu, kulinda haki yao ya kujitawala, na hatimaye kufurahia matunda ya maendeleo — ambayo yamekuwa hayapatikani kwa miaka mingi — watu wa Tigray lazima wajinasue kutoka kwenye mzunguko huu wa migogoro," alisema Abiy kupitia mtandao wa X.

Aliongeza kuwa utawala huo utashughulikia ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na kusaidia watu waliokimbia makazi yao kurejea majumbani mwao.

Tigray bado haijarudi katika hali yake ya kawaida kutokana na madhara makubwa ya kibinadamu yaliyotokana na vita vilivyopita.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi (UNHCR), kufikia mwezi Februari, takriban watu 750,000 kutoka Tigray walikuwa bado wakimbizi wa ndani, huku eneo hilo likikabiliwa na ukame unaohusishwa na hali ya hewa ya El Niño.

Mbali na Eritrea, serikali ya Ethiopia imezituhumu Misri na Sudan kwa kuunga mkono muungano huo wa waasi.

Nchi hizo zimekanusha tuhuma hizo.

CHANZO:reuters