Basi la abiria likiwa limedumbukia mtaroni nchini Kenya kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika ukanda wa Afrika Mashariki./Picha: Getty

Na Kevin Philips Momanyi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zimekumbwa na balaa la mafuriko yaliyosababisha vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu.

Mvua kubwa, zilizoambatana na upepo mkali zimeharibu kila kitu njiani mwake, huku mamlaka za nchi hizi husika, zikilazimika kuchukua hatua stahiki kuepusha madhara zaidi.

Hivi karibuni, Serikali ya Tanzania ilitoa tangazo la kufunga baadhi ya shule binafsi zilizo kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo.

Athari mbaya

Akihutubia bunge la taifa la nchi hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kuongezeka kwa idadi ya vifo vilivyotokana na mafuriko hayo. Kulingana na Majaliwa, vifo hivyo vimeongezeka kutoka watu 58 hadi 162, huku maafa zaidi yakiripotiwa katika maeneo ya Rufiji, Mwanza, Simiyu na Arusha.

Hii inakuja miezi minne baada ya nchi hiyo kukumbwa na maporomoko ya udongo kutoka Mlima Hanang, wilayani Hanang mkoani Manyara, tukio ambalo liliua zaidi ya watu 90.

Wakati huo huo, watu 70 wamepoteza maisha nchini Kenya kuanzia katikati ya mwezi wa Machi kutokana na mafuriko ambayo yameathiri zaidi ya watu 80,000, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Mafuriko hayo yamechochewa na kupasuka kwa kingo za Mto wa Athi na kulifanya sehemu kubwa ya jiji la Nairobi kumezwa na maji huku miundombinu na mali za watu zikiwa katika hali mbaya.

Madhara hayo yamemuibua kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga ambaye sasa anamtaka Rais William Ruto kutangaza mafuriko hayo kama janga la taifa.

Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Burundi ambapo watu takriban 200,000 wameathirika, huku nyumba zaidi ya 19000 na madarasa 209 yakisombwa na maji.

Nchini Somalia, watoto wanne wanaripotiwa kupoteza maisha wiki iliyopita, huku zaidi ya watu 800 wakiwa wameyakimbia makazi yao kutokana na mafuriko hayo.

Hali si tofauti kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inashuhudia ongezeko kubwa la viwango vya maji huku wananchi wakilazimika kuyahama makazi yao kuepuka madhara zaidi.

TRT Afrika