Bandari kavu Kwala

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema kuwa Bandari Kavu ya Kwala inatarajiwa kuanza kufanya kazi muda wowote kuanzia sasa.

Bandari hiyo inatarajiwa kutoa huduma zote za kiforodha kama zinavyo tolewa katika Bandari zingine. Na sehemu kubwa ya mizigo itakayo hudumiwa katika bandari hiyo ni ile inayokwenda nchi jirani kama vile Uganda, DRC, Rwanda, Burundi na kwingineko.

Takriban Shilingi bilioni 83.247 zimetumika katika kuendeleza bandari hiyo. Ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka barabara kuu ya Morogoro eneo la Vigwaza mpaka bandarini na kusogeza miundombinu ya reli mchepuko wenye urefu wa kilometa 1.3.

Tanzania imefafanua kuwa lengo kuu la kuanzisha bandari hiyo ni kuongeza pato la taifa lakini pia ufanisi hasa katika kiasi cha shehena zinazo hudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam na kupunguza msongamano.

Bandari hiyo ya Kwala ina uwezo wa kuhudumia wastani wa makasha 823 kwa siku sawa na makasha 300,395 kwa mwaka sawa na asilimia 30 ya makasha yote yanayo hudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.

TRT Afrika