Waziri wa Kilimo Tanzania Hussein Bashe amesema wameazimia kukomesha uwepo wa walanguzi ambao, kwa miaka mingi wametawala soko la sukari./Picha: TRT Afrika.

Serikali ya Tanzania imesema itaifungua biashara ya sukari kwa lengo la kuongeza ushindani na kuondoa wafanyabiashara wachache wenye mazoea ya kuhodhi bidhaa hiyo.

Hatua inakuja wakati serikali ya nchi hiyo inatarajia kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara 84 kwa tuhuma za ulanguzi wa sukari wa bidhaa hiyo ambayo imekuwa adimu nchini Tanzania.

Waziri wa Kilimo wa nchi hiyo Hussein Bashe amesema wameazimia kukomesha uwepo wa watu wa namna hiyo ambao, kwa miaka mingi wametawala soko la Sukari.

"Kuna baadhi ya wauzaji wamekuwa na tabia ya kuficha bidhaa hiyo ili kuongeza bei, atanunua kwa shilingi 2,800 na kuwauzia watu kwa shilingi 4,000 kwa kilo," amesema Bashe, wakati akijibu maswali ya wanahabari katika Ikulu ya Tanzania, mjini Dar es Salaam.

Kulingana na Bashe, wafanyabiashara 84 wameshakamatwa katika operesheni maalumu inayolenga kuwaondoa watu wenye tabia ya kuhodhi bidhaa hiyo.

Katika hatua nyingine, Bashe amesema Tanzania itaendelea kuagiza Sukari kutoka nje ya nchi mpaka mwisho wa mwaka 2024.

Waziri huyo amebainisha kuwa Tanzania ina mpango wa kuagiza zaidi ya ya tani 300,000 kupitia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA).

"Kama sio mabadiliko ya tabia nchi, Tanzania isingekuwa inapitia changamoto hii," amesema.

Hata hivyo, Bashe aliwahakikishia Watanzania kuwa hali ya upatikanaji wa sukari itatengemaa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Tanzania ina jumla ya viwanda saba vya sukari, vikubwa kati ya hivyo ni Kilombero, ambayo kwa siku inazalisha tani 700 za sukari, hata hivyo kiwango kimeshuka hadi 250, TPC kwa siku tani 450 lakini kwa sasa kimesimamisha uzalishaji kutoka na hitilafu za mashine, huku Kagera Sugar ikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 500 kwa siku, lakini sasa inazalisha wastani wa tani 200 hadi 300. Viwanda vyengine ni Mtibwa na Bagamoyo, ambapo kwa mujibu wa serikali, kutokana na mvua kubwa zinazoendelea, uzalishaji umepungua kwa takriban tani elfu moja kwa siku.

TRT Afrika