Moshi unaotoka Rafah baada ya kushambuliwa na vikosi vya Israeli. / Picha: Reuters

Umoja wa Afrika umelaani hatua ya jeshi la Israeli kuingia Rafah kusini mwa Gaza siku ya Jumatano, ukitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kukomesha "uchochezi mbaya" wa vita.

Mkuu wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat "analaani vikali kuenezwa kwa vita hivi hadi kwenye kivuko cha Rafah", ilisema taarifa, baada ya vifaru vya Israel kutawala njia muhimu ya kupitisha misaada ya kibinadamu Gaza iliyozingirwa.

Faki "anaonyesha wasiwasi wake mkubwa katika vita vilivyoanzishwa na Israeli huko Gaza ambavyo vinasababisha, kila wakati, vifo vingi na uharibifu wa utaratibu wa hali ya maisha ya binadamu," ilisema taarifa hiyo.

"Anatoa wito kwa jumuiya nzima ya kimataifa kuratibu ipasavyo hatua za pamoja ili kukomesha uchochezi huu hatari."

Makubaliano ya kusitisha mapigano

Uvamizi dhidi ya Rafah, ambapo kumejaa raia waliokimbia makazi yao, ulikuja wakati wapatanishi walipokutana mjini Cairo ili kujaribu kupata suluhu katika vita zinazoendelea kwa miezi saba.

Siku ya Jumatano, Israeli ilisema kuwa imefungua tena kivuko cha mpaka cha Kerem Shalom kuruhusu msaada wa kibinadamu kuingia Gaza, siku nne baada ya kukifunga kufuatia shambulio la roketi lililoua wanajeshi wanne.

Israeli pia ilisema kivuko cha mpaka cha Erez kati ya Israel na kaskazini mwa Gaza pia kiko wazi kwa ajili ya kupeleka misaada katika eneo la Palestina, kwa mara ya kwanza tangu vita hivyo kuanza.

Umoja wa Mataifa na mshirika mkuu wa Israel Marekani zote zililaani kufungwa kwa vivuko hivyo ambazo ni njia ya pekee ya kuwaingizia vyakula raia wanaokabiliwa na baa la njaa.

TRT Afrika