Tanzania ina sehemu kubwa zaidi ya Ziwa Victoria, ziwa kubwa zaidi barani Afrika, na hivi karibuni imeshuhudia ajali mbaya za boti Picha: Reuters

Mwili wa mtoto wa kike ambaye ni kati ya watu 13 waliozama majini baada ya mitumbwi miwili kuzama Ziwa Victoria katika pwani ya Kijiji cha Mchigondo Wilaya ya Bunda, Tanzania, umeopolewa.

Mwili huo umeopolewa baada ya saa 7 mchana Jumanne Agosti 1, 2023 na vikosi vya uokoaji vinavyoundwa na Askari wa Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi Kikosi cha Maji na wavuvi, siku tatu tangu ajali hiyo itokee.

Operesheni za kuopoa zinaendelea baada ya watu 13 wakiwemo watoto 11 kuhusika katika ajali kwenye ufuo wa Ziwa Victoria.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema kasi ya uokoaji imeongezeka leo baada ya kuwasili kwa boti mbili za kisasa na askari wazamiaji 22 kutoka mikoa ya Mara na Mwanza.

Kilichotokea

Inahofiwa walikuwa wamebeba uwezo wao maradufu na kusababisha ajali. Abiria hao pia wanashukiwa kuwa hawakuvaa jaketi la kuokoa maisha.

Afisa wa eneo hilo amelaumu ukosefu wa vifaa kwa kasi ndogo ya shughuli za uokoaji.

"Wamiliki wa boti wanatakiwa kuzingatia sheria na kanuni, hasa kuangalia uwezo wa meli na umiliki wa vifaa vya uokoaji wakati wa majanga," Mkama Nyamkinda alikiambia chombo cha habari cha ndani.

Tanzania ina sehemu kubwa zaidi ya Ziwa Victoria, ziwa kubwa zaidi barani Afrika, na hivi karibuni imeshuhudia ajali mbaya za boti zinazosababishwa zaidi na mizigo kupita kiasi na utunzaji duni wa meli.

Mnamo mwaka wa 2018, MV Nyerere - kivuko chenye uwezo wa kubeba watu 101 - kilizama kwenye ziwa na kuua watu 300. Takriban miili 138 ilitolewa ziwani.

TRT Afrika na mashirika ya habari