Prof. Mohamed Hassan Abdulaziz (Katikati). | Picha: Chuo Kikuu cha Nairobi

Msomi maarufu wa lugha na Sosholojia kutoka Kenya Prof. Mohamed Hassan Abdulaziz, maarufu Badi Hassani amezikwa leo mjini Mombasa, nchini Kenya.

Profesa Mohamed amesifika pakubwa kwa mchango wake kwa Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA), na BAWAKI (Baraza la Wanataaluma wa Kiswahili Kenya).

Profesa Mohamed Hassan Abdulaziz alistaafu hivi majuzi akiwa Profesa wa idara ya Isimu na lugha, Chuo Kikuu cha Nairobi alipohudumu kuanzia 1978 na kusifika kwa kuwa mhadhiri mwandamizi na mwanzilishi mwenyekiti wa Idara mpya ya Isimu na lugha za Kafrikika na mkurugenzi wa taasisi ya diplomasia na mahusiano ya Kimataifa, chuo kikuu cha Nairobi.

Kuanzia mnamo 1960 hadi hivi majuzi, alishiriki makongamano ya kitaifa ya sanaa na lugha yaliyoandaliwa na mashirikia kama vile UNESCO. Miongoni mwa Warsha hizo ni warsha iliyofadhiliwa na UNESCO ya kusahihisha Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa lugha ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, Tanzania, mwezi Septemba, 1993. Pia aliweza kushiriki Kongamano la Kwanza la Dunia la Isimu ya Kiafrika lililofanyika Chuo Kikuu cha Swaziland, mwezi Julai, 1994.

Profesa Mohamed Hassan Abdulaziz alisimamia zaidi ya tasnifu hamsini za Uzamili katika kipindi cha miaka ishirini na mitano iliyopita, katika nyanja mbalimbali za ufafanuzi wa Lugha za Kiafrika, Lugha ya Kiswahili na fasihi.

Amefunza Chuo Kikuu cha London, Makerere, University College, London, Chuo kikuu cha Riyadh, Saudi Arabia, Japan, Uswidi, Ufaransa, Italia na mataifa mengine.

Miongoni mwa majukumu yake ya siku zilizopita yalikuwa ni kuhudumu kuwa Mhadhiri wa Isimu na Kiswahili - Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, miaka ya sitini.

Mchango wake na juhudi zake kwenye lugha ya Kiswahili hazikusahaulika na Mnamo 1990, alipokezwa Tuzo ya Kitaifa ya Urais (O.G.W) kwa Huduma za Kielimu alizozitoa.

Profesa huyo aliandaa majarida ya kitaaluma kwenye mikutano ya kimataifa akiangazia Isimu jamii, hasa matumizi ya lugha, upangaji lugha na uhandisi, upataji na matumizi ya lugha, lugha katika elimu, sera za lugha ya taifa, lugha kuhusiana na matukio mengine ya kijamii, na nyanja ya upanuzi wa istilahi.

  • Mjumbe, Baraza la Taifa la Kiswahili, chombo kilichopewa dhamana ya kukuza Kiswahili, ikijumuisha istilahi mpya, Tanzania, 1968 - 1970
  • Mjumbe wa Baraza la Kitaifa la Utamaduni la Kenya
  • Mwanachama wa Taasisi ya Kimataifa ya Afrika, London
  • Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti wa Bodi ya Mafunzo ya Kiswahili, Afrika Mashariki (RISSEA)
  • Mjumbe, Baraza la Taifa la Kiswahili, chombo chenye dhamana ya kukuza Kiswahili, ikijumuisha istilahi mpya, Tanzania, 1968 - 1970
  • Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Utafiti wa Lugha wa Afrika Mashariki 1967 - 1971

TRT Afrika