Faisal Halim alipata majeraha ya moto kwenye shingo, bega, mikono na kifua katika wilaya ya Petaling Jaya nje ya mji mkuu Kuala Lumpur mwishoni mwa wiki. / Picha: Reuters

Mchezaji wa Timu ya Taifa ya soka ya Malaysia ambaye alikuwa muathirika wa shambulio la tindikali yuko katika hali ya "hatari" na kuchomeka kwa kiwango cha nne ambacho kinahitaji upasuaji zaidi, afisa wa soka aliiambia AFP.

Mkuu wa polisi wa jimbo la Selangor Hussein Omar Khan aliwaambia waandishi wa habari kuwa uchunguzi kuhusu kiini cha shambulio hilo unaendelea na kwamba washukiwa wawili wamekamatwa.

Nyota huyo, maarufu kwa jina la utani "Mickey," mwenye umri wa miaka 26 anacheza kama kiungo kulia katika klabu ya Soka ya Selangor na timu ya taifa ya Malaysia.

Afisa mkuu mtendaji wa klabu ya Selangor Johan Kamal Hamidon amesema kuwa usalama umeimarishwa kwa wachezaji, viongozi na wafanyakazi wa klabu hiyo bila kutoa maeleza zaidi.

Rais wa Shirikisho la Soka la Malaysia Hamidin Mohamad Amin amewahimiza wachezaji wa soka katika ligi ya juu kuchukua tahadhari kuhusu usalama wao binafsi, ikiwa ni pamoja na kuajiri walinzi.

Shambulio hilo la asidi lilijiri siku tatu baada ya mchezaji mwengine wa timu ya taifa, Akhyar Rashid, kujeruhiwa katika tukio la uporaji nje ya nyumba yake iliyoko katika jimbo la Mashariki la Terengganu.

Mkuu wa polisi wa Kuala Lumpur Terengganu Azli Mohamad Noor amesema kuwa matukio hayo hayana uhusiano.

AFP