Mkesha huo ulifanyika Jumamosi. Picha: TRT Afrika.

Makumi ya Wakenya wamefanya mkesha unaounga mkono Wapalestina katika mji mkuu Nairobi, wakilaani kuendelea kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza.

Walitoa maombi kwa wale ambao wamepoteza maisha katika shambulio la mabomu linaloendelea Gaza. Tukio hilo lilifanyika Jumamosi usiku.

"Tumekusanyika ili kukemea ukandamizaji unaowakabili watu wa Palestina na Israel na kupeleka maombi yetu ya dhati kwa wale ambao wamepoteza maisha yao," Rasha Al Jundi, mmoja wa waandalizi wa hafla hiyo anayewakilisha shirika la Kenya kwa Palestina alisema.

Zaidi ya watu 50 walihudhuria hafla moja jijini Nairobi. Picha: TRT Afrika

Rasha alitoa wito wa'' kususia bidhaa za Israel'' na biashara nchini Kenya kama njia ya kupinga vitendo vya Israel.

''Wengi wetu tunasimama na watu wa Palestina," Kennedy Wanga, aliyehudhuria mkesha huo alisema.

Waliokuwepo kwenye hafla hiyo ya mkesha wamelaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza. Picha: TRT Afrika.

Kumekuwa na wasiwasi wa kimataifa kuhusu hali ya Gaza huku Israel ikiendelea na mashambulizi yake ya anga dhidi ya Wapalestina.

Siku ya Ijumaa kulifanyika maombi maalum kwa ajili ya Wapalestina katika baadhi ya Misikiti nchini Kenya huku Maimamu wakiilaani Israel kwa hatua yake dhidi ya Gaza.

TRT Afrika