Serikali ya Rwanda imeyapiga marufuku mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini humo kushirikiana na Ubelgiji.
Mamlaka ya nchi hiyo imezitaka NGOs na taasisi zingine, kuacha mara moja kushirikiana na serikali ya Ubelgiji.

“Kuanzia sasa, taasisi zote zisizo za kiserikali pamoja na programu zingine, hazitoruhusiwa kushirikiana na serikali ya Ubelgiji,” ilisema taarifa iliyotolewa na serikali ya Rwanda.
Hatua hiyo ni muendelezo wa dosari ya mahusiano kati ya nchi hizo mbili hasa baada ya Rwanda kusitisha uhusiano wake na Ubelgiji mwezi mwaka huu.
Kulingana na Rwanda, miradi yoyote ya ushirikiano kati ya taasisi hizo na Ubelgiji inapaswa kusitishwa mara moja.
Serikali ya Rwanda ilisisitiza kuwa hapatakuwa na msaada wowote utakaopelekwa Ubelgiji wala kupokelewa kutoka nchi hiyo.
Rwanda imeonya kuwa hatua kali za kinidhamu zitatolewa kwa taasisi zozote zitakazokaidi amri hiyo.

Machi 17 mwaka huu, Rwanda ilisitisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Ubelgiji, na kutoa saa 48 kwa wanadiplomasia wa nchi hiyo kuondoka nchini humo.
Rais Paul Kagame ameituhumu Ubelgiji kwa kuchochea vikwazo vya kimataifa dhidi ya nchi yake, kufuatia machafuko yanayoendelea Mashariki mwa DRC.







.jpg?width=512&format=webp&quality=80)












