Maafisa watatu wa polisi wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya washukiwa wa ujambazi kuwashambulia wakiwa kwenye doria yao katika jimbo la kaskazini magharibi la Katsina nchini Nigeria siku ya Jumanne, polisi walisema siku ya Jumatano.
Mashambulio hayo yanaongeza idadi ya matukio ya hivi karibuni, ikiwemo utekaji nyara wa magenge yenye silaha walio katika misitu.
Msemaji wa polisi wa jimbo la Katsina Abubakar Sadiq Aliyu alisema maafisa hao walishambuliwa vibaya asubuhi wakiwa katika doria kwenye barabara ya Guga-Bakori.
Maafisa hao "walipambana kishujaa,” kukabiliana na mashambulizi hayo, lakini watatu wao wakauawa katika shambulio hilo, Aliyu alisema katika taarifa.
Polisi wawili waliojeruhiwa wanaendelea kutibiwa katika hospitali ya karibu, alisema.














