Serikali ya Uganda siku ya Jumanne ilikanusha madai kwamba inawalenga wapinzani wa kisiasa kufuatia uchaguzi wa urais uliofanyika wiki iliyopita.
Katika taarifa yake, Waziri wa Habari Chris Baryomunsi alikiri kukamatwa kwa watu, lakini akasema waliokamatwa ni wale waliokuwa wamesababisha “matatizo.”
Siku chache tu baada ya uchaguzi wa Januari 15, vyombo vya usalama viliripotiwa kuongeza msako dhidi ya wafuasi wa upinzani.
Kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, amejificha tangu Rais Yoweri Museveni, atangazwe mshindi wa uchaguzi wa urais.
Matokeo rasmi yalionyesha Museveni akishinda kwa asilimia 71 ya kura, huku Bobi Wine akipata asilimia 24. Bobi Wine alipinga matokeo hayo akiyataja kuwa “ya uongo,” akidai kulikuwa na udanganyifu wa uchaguzi. Hata hivyo Tume ya uchaguzi haijajibu madai hayo.
Waliokamatwa
Waziri wa Habari alieleza kuwa kulikuwa na makundi mawili ya waliokamatwa. Kundi la kwanza lilihusisha wale “waliotaka kusababisha vurugu kwa sababu mgombea waliomuunga mkono alishindwa katika uchaguzi,” na kundi la pili lilihusisha “magenge ya kihalifu yaliyohamasishwa na viongozi wao kutumia kipindi cha uchaguzi kama fursa ya kuanzisha machafuko ya kiraia nchini.”
“Wale waliokuwa wanapanga aina hiyo ya vurugu wamekamatwa, na wale walioko mafichoni watapatikana na kukamatwa kulingana na sheria,” aliongeza Baryomunsi.
Bobi Wine amedai kuwa wafuasi wake walikuwa wanalengwa, akisema kupitia mitandao ya kijamii kwamba zaidi ya watu 100 waliuawa katika vurugu zinazohusiana na uchaguzi, bila kutoa ushahidi.
Kauli zake zilifuatia matamshi ya mkuu wa jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba — mwana wa Museveni — aliyesema kuwa vikosi vya usalama viliua “magaidi” 22 wa upinzani wakati wa vurugu zilizohusiana na uchaguzi.
Viongozi wa upinzani kutoweka
David Lewis Rubongoya, katibu mkuu wa chama cha National Unity Platform (NUP) cha Bobi Wine, alisema kuwa viongozi kadhaa wa chama hicho hawajulikani walipo na wengine wamekamatwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Katika hotuba yake ya ushindi siku ya Jumapili, Museveni alikitaja chama cha NUP kuwa cha “kigaidi,” akiishtumu chama hicho kujaribu kutumia vurugu kubatilisha matokeo ya uchaguzi.













