| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mlio wa mabomu, sauti za risasi zasikika mji mkuu wa Niger karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa
Wakazi katika maeneo jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani wamesema kwamba ufyatuaji wa risasi umeendelea kwa takriban saa mbili kabla ya kuacha.
Mlio wa mabomu, sauti za risasi zasikika mji mkuu wa Niger karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa
Niger tangu mwaka 2023 imetawaliwa na Jenerali Abdourahamane Tiani. / Reuters
tokea masaa 6

Sauti za milio ya risasi na milipuko imesikika muda mfupi usiku wa kuamkia Alhamisi karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa uliopo mjini Niamey nchini Niger, hali iliyoogopesha wakazi wa mji huo.

Video zilizopigwa na wakazi zimeonesha mwanga angani, pamoja na sauti za milipuko.

Picha nyengine ambazo zimesambaa mitandaoni zimeonesha moshi ukipanda juu angani huku magari kadhaa yakichomwa.

Wakazi katika maeneo jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Diori Hamani wamesema kwamba ufyatuaji wa risasi umeendelea kwa takriban saa mbili kabla ya kuacha.

Kufikia saa nane usiku, hali ya utulivu ilirejea.

Uwanja wa ndege ambao ni kilomita 10 kutoka Ikulu, una kambi ya kikosi cha anga na ni kituo cha mkakati cha kijeshi.

Pia ni makao makuu ya vikosi shirikishi kati ya Niger, Burkina Faso na Mali kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel.

Mamlaka, mpaka kufikia mapema Alhamisi, haijatangaza chanzo cha vurugu hizo na iwapo kuna waliojeruhiwa.

Wakazi kadhaa waliripoti kusikia sauti za ving'ora huku magari ya zima moto yakielekea uwanja wa ndege asubuhi mapema.

Niger tangu 2023 imetawaliwa na Jenerali Abdourahamane Tiani, kufuatia kupinduliwa kwa serikali iliyochaguliwa madarakani.

Tangu wakati huo, nchi hiyo ilivitimua vikosi vya Ufaransa na Marekani ambavyo awali vilisaidia kupambana na ugaidi.

Wito wa "kuingia mitaani kutetea nchi”

Mwanaharakati wa mitandaoni ambae anaunga mkono serikali, Ibrahim Bana, ameweka video katika mtandao wa Facebook akiwataka wananchi kuingia mitaani "kulinda nchi," na kuibua hali ya wasiwasi.