Ghana imempa uraia mtengeneza maudhui ya YouTube Mmarekani IShowSpeed, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo ametangaza, huku mtengeneza maudhui akikamilisha ziara ya mwezi mzima ya barani Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje Sam Okudzeto Ablakwa alisema katika mtandao wa kijamii wa X kuwa "baada ya kuthibitisha uhusiani wa dhati wa IShowSpeed na Ghana", serikali yake "imeidhinisha kumpa pasi ya kusafiria ya Ghana IShowSpeed."
"Endelea kulipa fahari taifa letu tukufu la Ghana, na bara letu zuri la Afrika. Ghana inakuenzi," waziri huyo alisema.
IShowSpeed, Mmarekani mweusi mwenye umri wa miaka 21 – aliyezaliwa Cincinnati, Ohio kama Darren Jason Watkins Jr. – ni mtengeneza maudhui wa mwenye ushawishi mkubwa mitandaoni.
Afrika iliyo tofauti
Katika ziara yake ya Afrika alifika jumla ya wafuasi milioni 50 kwenye YouTube mwezi huu. Shirika la Forbes linakadiria thamani yake kuwa dola milioni 20.
Ziara ya IShowSpeed, ambayo ilianza Disemba 29, imemfikisha katika nchi 20, na kuonesha mamilioni ya wafuasi wake taswira tofauti ya bara la Afrika wakati akifanya ziara katika migodi ya almasi ya Botswana, vyakula vizuri vya Ethiopia na kuhudhuria fainali za AFCON nchini Morocco.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanasema IShowSpeed ameonesha Afrika iliyo tofauti, tofauti na taswira hasi inayooneshwa katika televisheni.














