| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Eritrea yakataa raia wake kurejeshwa kwa lazima kutoka Uingereza
Serikali ya Uingereza imetishia kupiga marufuku raia wote wa Eritrea kuingia nchini humo, iwapo Eritrea haitakubali kupokea raia wake wakiwemo wale waliofika Uingereza kwa kutumia njia zizizo rasmi au wale waliohukumiwa kwa makosa ya jinai.
Eritrea yakataa raia wake kurejeshwa kwa lazima kutoka Uingereza
Eritrea imeishutumu Uingereza kwa kufanya mfumo wake wa hifadhi ya ukimbizi kuwa suala la kisiasa

Serikali ya Eritrea inasema haikubali kurejeshwa kwa lazima kwa raia wake, na inasisitiza kuwa imewasilisha msimamo huo kwa serikali ya Uingereza mara kadhaa.

Serikali ya Uingereza imetishia kupiga marufuku raia wote wa Eritrea kuingia nchini humo, mpaka Eritrea itakapokubali kupokea raia wake zaidi—wakiwemo wale waliofika Uingereza kwa kutumia boti ndogo au wale waliohukumiwa kwa makosa ya jinai—kama ilivyoelezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shabana Mahmood, siku ya Alhamisi.

"Eritrea imepata fursa zote za kukubali kurejeshwa kwa wahalifu na wale wasio na haki ya kuwepo nchini Uingereza. Tofauti na nchi nyingine, imekataa kufanya hivyo," alisema, huku akiongeza kuwa atazingatia kuchukua hatua zaidi dhidi ya nchi zinazokataa kushirikiana.

Katika taarifa iliyotolewa na ubalozi wake nchini Uingereza, Eritrea imeeleza kuwa Uingereza haijaonyesha nia yoyote ya kushiriki katika mazungumzo yenye tija.

"Badala yake, inaendelea kusisitiza kurejeshwa kwa watu kwa lazima, jambo ambalo linakinzana moja kwa moja na Sera yake yenyewe ya Mwongozo kuhusu Eritrea," inasema taarifa hiyo.

Kuanzia Alhamisi, serikali ya Uingereza imesema wanadiplomasia wa Eritrea watakabiliwa na vikwazo katika harakati zao nje ya London, huku utaratibu wa kutoa viza kwa haraka kwa maafisa wa ngazi za juu na watu wengine mashuhuri ukisitishwa.

Chini ya hatua hizi mpya, wanadiplomasia wa Eritrea hawataruhusiwa kusafiri umbali unaozidi kilomita 60 nje ya London bila kupata kibali.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imesema vikwazo hivi vinafanana na vile vilivyowekwa kwa maafisa wa Uingereza katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara.

Eritrea imeishutumu Uingereza kwa kufanya mfumo wake wa hifadhi ya ukimbizi kuwa suala la kisiasa, na kutoa hifadhi kwa mtu yeyote anayedai kuwa raia wa Eritrea, kwa lengo la kudhoofisha serikali ya Eritrea.

Serikali ya Uingereza imewashutumu maafisa wa Eritrea kwa kusitisha ushirikiano ghafla mapema mwaka huu.

Eritrea katika taarifa imesema ililazimika kusitisha utaratibu wa kusindikiza raia wake waliokuwa wakirejea nchini mwao, ambao inadaiwa walikuwa wakirejea 'kwa hiari' baada ya kugundua wengi walikuwa wafungwa.

"Kutokana na vitendo visivyokubalika vya mamlaka za Uingereza—kama vile kushindwa kufichua kuwa walikuwa wakirejesha wahalifu waliohukumiwa ambao bado walikuwa wakitumikia vifungo, na kudai kuwa watu hao wanarejea 'kwa hiari' wakati ukweli ni kwamba hawakurejea kwa hiari,” Eritrea inaongeza katika taarifa yake.

CHANZO:TRT Swahili