Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ameteuliwa kuongoza Timu ya Pamoja ya Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD) itakayoshughulikia mchakato wa amani nchini Sudan Kusini.
Kamati hiyo inaundwa na Marais wa Afrika Kusini, Nigeria, Rwanda, Algeria na Chad, na pendekezo la kuundwa kwa timu hiyo lilitolewa katika mkutano uliofanyika Septemba 29, 2026.
Akizindua timu hiyo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ameeleza matumaini kuwa ushirikiano baina ya taasisi hizo za kimataifa utasaidia kuharakisha mchakato wa kuleta amani ya kudumu nchini Sudan Kusini.
Itakumbukwa kwamba Kikwete, pia ni Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika katika Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.
Sudan Kusini iko katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ambao baada ya tarehe yake ya awali kuahirishwa, hivi sasa umepangwa kufanyika mwezi Februari 2027. Hata hivyo, nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa fedha kwa ajili ya maandalizi ya zoezi hilo muhimu katika historia yake.
Wito umetolewa kwa nchi kadhaa kuisadia Sudan Kusini ili kufikia malengo yake yanaonekana ndio yatakuwa chachu kubwa ya kuleta utulivu wa kisiasa nchini humo.













