Baadhi ya nyumba zikiwa zimefunikwa kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania./Picha: Red Cross Tanzania.

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Zaidi wa watu 100 wamepoteza maisha kufuatia mvua za El Nino na mafuriko yaliyoikumba Tanzania, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa amesema.

Majaliwa amesema zaidi ya kaya 51,000 na watu 200,000 wameathirika na mvua hizo, huku watu 162 wakipoteza uhai wao na wengine 236 kujeruhiwa.

"Zikiwa zimeambatana na upepo mzito na maporomoko ya udongo, mvua hizi zimeleta athari kubwa nchini," amesema Majaliwa wakati anahutubia Bunge la Taifa la nchi hiyo jijini Dodoma, Tanzania, siku ya Alhamisi.

Kulingana na Majaliwa, mbali na vifo, mvua hizo pia zimesababisha uharibifu wa mazao, mali na miundombinu mingine kama vile madaraja, reli na barabara.

Shule kufungwa

Wakati huo huo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania imetangaza kufungwa kwa muda kwa shule binafsi zilizoathirika na mvua za El Nino.

Katika taarifa yake iliyosainiwa na Kamishna wa Elimu katika Wizara hiyo Dkt Lyabwene Mtahabwa, wizara hiyo imesema imefanya ufuatiliaji wa haraka na kubaini kuwa miondombinu ya baadhi ya shule ikiwemo kubomoka na kuezuliwa kwa mapaa ya shule, vyo kutitia, yumba za walimu kubomoka na barabara kuja mali, hali inayopelekea kufungwa kwa barabara hizo na viwanja vya shule kujaa maji.

Sehemu ya taarifa iliyotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania./Picha: Wizara ya Elimu-Tanzania

"Kwa kuzingatia jali ya mvua inayoendelea sasa, Wizara inaomba iwajulishe wamiliki wa shule binafsi walio chini yako, ambao shule zao zimepata athari ya mvua zinazoendelea, kufanya tathmini ya athari zilizotokana na mvua hizo na endapo athari ni kubwa, shule husika zichukue hatua za haraka za kufunga shule kwa muda kwa kuzingatia hali halisi ili kulinda uhai wa wanafunzi na walimu wao," imesomeka sehemu ya taarifa hayo.

Wanafunzi 8 wa shule ya Ghati Memorial ya mkoani Arusha, Tanzania walipoteza maisha baada ya gari lao la shule kusombwa na maji, siku ya Aprili 12, 2024.

TRT Afrika