Gavana wa Kenya, atishia kuajiri madaktari kutoka Uganda

Gavana wa Kenya, atishia kuajiri madaktari kutoka Uganda

Raia wa Kenya wanahaha kupata matibabu huku mgogo wa madaktari ukiingia siku ya 43.
Madaktari waapa kutorudi kazini hadi matakwa yao yote yatimizwe. / Picha: Wengine

Huku vuta n’kuvute kati ya serikali na madaktari ukiendelea nchini Kenya, Gavana wa Transzoia, George Natembeya atishia kuajiri madaktari kutoka Uganda ikiwa madaktari wa kutoka Kenya, hawatorudi kazini.

"Tutaanza kwa kusimamisha mishahara yao mwisho wa mwezi huu, halafu kuanzia mwezi ujao, nitaenda Uganda kutangaza nafasi ya kazi ya madaktari. Kwa sababu itifaki za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinasema kuna uhuru wa watu kufanya kazi, kufanya biashara na kutoa huduma. Hii ina maana kwamba nikiwa na nafasi za kazi, watakuja hapa hata kama hawahitaji vyeti tu," alisema gavana huyo wa Transzoia.

Alisema madaktari wanapaswa kurudi kazini, kwa sababu matakwa yao yashatekelezwa.

“Nimetekeleza matakwa yote ya madaktari isipokuwa kupandishwa cheo kwa madaktari tisa ambayo Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti inashughulikia. Tulifanya uamuzi muda mrefu uliopita na kupandishwa cheo kwao kunasubiriwa na bodi. Tayari tumewapandisha vyeo 30,” alisema Natembeya.

Pia alitoa wito kwa madaktari warudi kazini kwa haraka au kupoteza kazi zao.

"Wahudumu wote wa afya wanaogoma watakosa mishahara yao ya Aprili na wana hatari ya kupoteza kazi zao kuanzia Mei ikiwa hawatarejea kazini katika maeneo yao ya kazi," alisema.

Vitisho kutoka Serikalini

Naye waziri wa utumishi wa umma Moses Kuria alitishia kutowalipa madaktari wanaogoma.

Waziri huyo ametishia kutolipa madaktari wanaogoma na kubadili masharti ya ajira kutoka ya kudumu na ya pensheni hadi ya ule wa mikataba.

Aidha alitoa wito kwa wananchi kuwataka madaktari kuheshimu maagizo ya mahakama ya kusitisha maandamano.

Kuria alisema, "nilitarajia wananchi kuuliza madaktari vilevile wanavyotuuliza sisi kuheshimu maagizo ya mahakama. Mgomo huo ulisitishwa mara tatu na mahakama lakini hawakuheshimu. Ingekuwa ni serikali haikuheshimu maagizo, hii ingekuwa hadithi tofauti.

Matakwa ya Madaktari

Katibu Mkuu wa KMPDU ameapa kutolegeza kamba hadi pale matakwa yao yote yatekelezwe.

Wakizungumza na wanahabari, Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah na Naibu Katibu Mkuu Dennis Miskellah walishilia msimamo wa kutekeleza makubaliano ya 2017 kwa ujumla wake, likiwemo suala tata la fidia ya madaktari wanafunzi.

TRT Afrika