Upande wa Mashariki mwa nchi hiyo una kiwango cha chini cha kujua kusoma na kuandika ukilinganisha na upande mwingine wa nchi. Picha: UNICEF  

Na Kudra Maliro

Akiwa nchini ya turubai, Rufin Kambale anafundisha wanafunzi wa darasa la nne Jiografia katika Shule ya Msingi ya Sayo, mojawapo ya miundombinu ya muda katika jimbo la Kivu Kaskazini linalokumbwa na migogoro ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hata hivyo, suluhusho hili la muda mfupi lililojengwa na UNICEF bado halionekani kutosheleza.

Mashimo na matobo kwenye mapaa haya huruhusu kupita kwa miale ya jua na vumbi. Wanafunzi wanaweza kuwa wamezoea hili, lakini mwalimu wanawaona wanavyohangaika kufuatilia masomo katika hali hiyo .

"Ni ngumu sana kwa wanafunzi kuhudhuria masomo katika mazingira haya. Sio tu wanashindwa kufanya vizuri darasani, lakini pia huwa nyuma kimtaala," Rufin anaiambia TRT Afrika.

Hakuna ripoti za shule

Shule kadhaa katika eneo la migogoro zimefungwa kwa muda mrefu, na kuwalazimu wanafunzi kukaa nyumbani siku nzima au kufanya kazi zisizo za kawaida ili waweze kujikimu.

"Nimekosa masomo mara kwa mara tangu shambulio la kwanza katika kijiji chetu mwaka wa 2016," anasema Josias.

Kwa mujibu wa UNICEF, karibu watoto milioni moja wamekimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya waasi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini.

Josias, kama vijana wengine wengi ambao wamekimbia mashambulizi ya mara kwa mara na waasi wa ADF katika eneo la Beni, anatafuta hifadhi katika dawa za kulevya.

Wakati mwingine, yeye huuza viatu ili kupata riziki, akiweka kando ndoto yake ya kuwa daktari.

Ripoti zake zote za shule ziligeuka majivu wakati kijiji chake kiliposhambuliwa.

Mgogoro wa kisiasa katika eneo la Mashariki la DRC limesababisha karibu watoto milioni kukosa makazi, kulingana na Umoja wa Mataifa./Picha: UNICEF

Kilio cha Msaada

Hali ya kiakili ya Josias inaakisi ile ya watoto wengi wadogo katika shule za waliohamishwa.

Esdras Kambasu, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Beni, anadokeza kuwa wanafunzi wengi huwa kama wamechanganyikiwa wawapo darasani. Angependa kuona mifumo maalum ya msaada kwa watoto hawa.

"Wanafunzi waliohamishwa wanafuata mkondo sawa na watoto wengine. Wananufaika na elimu ya bure lakini mara nyingi wako nyuma ya mtaala wa kitaifa. Ili kufikia hatua hiyo, kila mzazi anaweza kumlipia mtoto wao mkufunzi. Lakini hiyo inafanya mfumo kutokuwa sawa," aniambia TRT Afrika.

Wakati wa ziara yake nchini DRC, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk anasema ni vyema dunia ikazinduka na kuchukua hatua kuzuia yanayoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Takriban watu 300,000 wamekimbilia mji wa Goma na maeneo jirani. Wakati mapigano yakiendelea, mzozo wa kibinadamu unazidi kuwa mbaya, na kuzidisha hali ya watu wasio wa kawaida milioni 7.2 ambao tayari wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia.

Kuwawinda waasi

"Tutaendelea kutetea haki za binadamu, hasa haki za watu waliokimbia makazi yao," anasema Türk.

Wanafunzi wengi wanakosa huduma za muhimu za elimu kama sehemu za kusomea, madawati na madaftari. Picha: UNICEF

Kwa kukosa chakula cha kutosha inamaanisha watoto hawa wanakuja shuleni wakiwa na njaa sana ili kuzingatia masomo yao. Ni mzunguko mbaya ambao hufanya juhudi za kibinadamu kuwa changamoto zaidi.

Walimu wengi pia wamehama makazi kutokana na ukosefu wa usalama na kuwaacha wakihangaika sawa na watoto.

Mara kwa mara, serikali ya DRC imekuwa ikiituhumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, tuhumu ambazo zimekanwa na Rwanda.

Hali kadhalika, Kinshasa imehitimisha shughuli ya kulinda amani ya majeshi ya Afrika Mashariki, na kukishutumu kwa kushindwa kukabiliana na waasi.

Disemba 2023, DRC iliomba msaada kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) "kuwaunga mkono katika jitihada za kurejesha amani Mashariki mwa DRC".

Tumaini la amani

Kikosi hichi kinachojumusha majeshi kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania, vimepelekwa DRC kupambana na makundi ya watu wenye silaha, wakiwemo M23.

Pamoja na uwepo wa vita, bado wanafunzi wana mategemeo ya kurejea madarasani.Picha: UNICEF

Pamoja na mashambulizi ya waasi, wanafunzi bado wana mategemeo ya kurejea madarasani, kama ilivyokuwa hapo awali.

Rose Batumike, msichana mwenye umri wa miaka 17 ambaye ameishi katika kambi ya Goma tangu akikimbia mashambulizi ya M23 huko Rutsuru, hakati tamaa na ndoto yake ya kurejea shuleni ili kupata shahada yake.

"Serikali ya Kongo iwawinde waasi hawa haraka iwezekanavyo ili nirudi nyumbani kuendelea na masomo...sijui lolote kuhusu siasa. Nia yangu pekee ni amani irudi DRC," anaiambia TRT Afrika.

TRT Afrika