| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Sudan Kusini inahitaji “hatua za dharura” ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba “nidhamu ya kijeshi inaonekana kuporomoka” kwa pande zote za mzozo.
Sudan Kusini inahitaji “hatua za dharura” ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe
Makabuliano ya kugawana madaraka kati ya Rais Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar umesambaratika. / / Reuters
tokea masaa 5

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa alitoa tahadhari siku ya Ijumaa kuhusu hali inayozorota nchini Sudan Kusini, akitaka “hatua za dharura” ili kuzuia kurejea kwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.

“Tunahitaji hatua za dharura kulinda makubaliano ya amani na kuzuia mgawanyiko na mizunguko ya kulipizana kisasi ambayo inaweza kuashiria kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe,” alisema Volker Turk katika hotuba yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Ghasia zimeongezeka katika wiki za hivi karibuni huku makubaliano ya kugawana madaraka kati ya viongozi hasimu, Salva Kiir na Riek Machar, yakivunjika.

Tangu Disemba, angalau watu 280,000 wamekimbia makazi yao katika jimbo lililoathirika zaidi la Jonglei.

Turk alionya kuwa hali ilizorota zaidi mnamo Januari, huku “ukiukwaji na unyanyasaji wa haki za binadamu ukiongezeka kwa asilimia 45” ikilinganishwa na mwezi uliotangulia.

Mwezi uliopita pekee, alisema ofisi yake ilirekodi kuwa raia 189 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Mkuu huyo wa haki za binadamu alisema “alishtushwa” kusikia kuhusu shambulio la wikendi iliyopita lililofanywa na majeshi ya serikali pamoja na wanamgambo washirika dhidi ya kijiji katika Kaunti ya Ayod, Jonglei.

Watuu kadhaa wauawa

“Mashahidi waliwaeleza wenzangu kwamba wanajeshi waliwaamuru wakazi wakusanyike pamoja, kisha wakawafyatua risasi, na kuua raia 21 wasio na silaha wakiwemo wanawake na watoto,” Turk alisema.

Alionya kwamba “nidhamu ya kijeshi inaonekana kuporomoka” kwa pande zote za zinazozozana, huku wanajeshi wakionyesha “kupuuza ulinzi wa raia.”

Alisema maafisa wake walirekodi ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa mwaka 2024 katika mzozo huo mwaka jana, hadi kufikia zaidi ya 5,100.

Turk alieleza wasiwasi wake hasa kuhusu hotuba za chuki na uchochezi wa vurugu unaolenga jamii nzima na makabila mbalimbali nchini humo.

“Katika rekodi moja ya sauti iliyothibitishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa, afisa mwandamizi wa kijeshi aliwahimiza wanajeshi wake kutomsaza mtu yeyote hai, na kuharibu nyumba za raia, mifugo na mali,” aliliambia baraza hilo.

“Vitendo vya hotuba za chuki na uchochezi wa vurugu vinaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kimataifa,” Turk alisema, akionya kwamba “wale wanaohusika na uhalifu kama huo wanaweza kushtakiwa chini ya sheria za kimataifa.”

Mkuu huyo pia alionya kwamba Sudan Kusini imekuwa “hatari kupita kiasi kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu,” huku mashambulizi 350 dhidi ya wafanyakazi na vituo vyao yakiripotiwa mwaka jana — zaidi ya theluthi moja ya ongezeko ikilinganishwa na mwaka 2024.

 

CHANZO:AP