Burkina Faso imekuwa nchi ya hivi karibuni barani Afrika kusaini mpango huo wa afya unaozua mjadala mkubwa.
Hatua hii imeibua maswali mengi, si tu kwa sababu ya wasiwasi ulioenea kuhusu masharti ya mikataba kama hii, bali pia kutokana na msimamo wa Burkina Faso chini ya uongozi wa Rais Ibrahim Traore, ambayo katika miaka ya karibuni imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazojitenga na ushawishi wa mataifa ya Magharibi.
Inaripotiwa kuwa ufadhili huo wa Marekani, chini ya mkakati wa Trump unaojulikana kama “America First Global Health Strategy,” unahusishwa na kuipa Washington fursa ya kupata rasilimali za madini pamoja na kukusanya taarifa binafsi za kiafya za Waafrika. Hata hivyo, bado haijabainika wazi iwapo vipengele hivyo vyenye utata vimejumuishwa katika makubaliano kati ya Marekani na Burkina Faso.
“Kuhifadhi data kidijitali”
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa mpango huo unatarajiwa kusaidia “kuboresha na kuhifadhi data na takwimu kidijitali” pamoja na kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza “kabla hayajasambaa katika kanda au kufika Marekani.”
Burkina Faso bado haijatoa ufafanuzi rasmi kuhusu makubaliano hayo. Baadhi ya wachambuzi wanasema huenda hatua hiyo imetokana na juhudi za hivi karibuni za kidiplomasia za utawala wa Trump, ambao umeanza kushirikiana na nchi za Ukanda wa Sahel, tofauti na mtazamo wa utawala uliopita.
Burkina Faso ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika, na pia ina rasilimali nyingine za madini kama shaba, almasi na bauxite.
Tangu aingie madarakani mwaka 2022, Traore ameahidi kulinda rasilimali za nchi yake dhidi ya kile alichokiita unyonyaji “usio wa haki” kutoka kwa mataifa ya kigeni.
DRC nayo yakubali
Wakati huohuo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, taifa jingine lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, pia limesaini mpango huo wa afya wa Trump wenye thamani ya dola bilioni 1.2.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, jumla ya nchi 18 za Afrika zimekubali mpangi wa ufadhili wa Trump wa “America First” wenye thamani ya dola bilioni 18.
Nchi hizo ni: Botswana, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Côte d’Ivoire, Eswatini, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Liberia, Madagascar, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Sierra Leone, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda.
Hata hivyo, Zambia na Zimbabwe zimeripotiwa kukataa ufadhili huo kutokana na wasiwasi kuhusu kushiriki taarifa nyeti za kiafya na upatikanaji wa rasilimali za madini.
Mkurugenzi Mkuu wa Africa Centres for Disease Control and Prevention, Jean Kaseya, ameonyesha “wasiwasi mkubwa” kuhusu kushirikishwa kwa vimelea (pathogens) kama sehemu ya makubaliano hayo.
Utawala wa Trump, unaofuata sera ya mambo ya nje yenye misingi ya kimaslahi ya moja kwa moja, umesisitiza mara kadhaa kwamba ufadhili wa Marekani kwa mataifa ya nje haupaswi kuonekana kama “hisani,” bali lazima maslahi ya Washington yawe kipaumbele cha juu.













