Waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU) Jumanne walisema uchaguzi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako Rais aliye madarakani Faustin-Archange Touadera aliwania tena urais, umefanyika kwa amani.
Touadera, mwenye umri wa miaka 68, anatafuta muhula wa tatu na amekuwa na juhudi zake za kuhakikisha kuwepo kwa amani katika taifa.
Baadhi ya wanachama wa upinzani walitoa wito wa kususiwa kwa uchaguzi, wakisema mchakato ulikuwa si wa wazi na kutaka kufanyike mazungumzo ya kisiasa.
Touadera aliingia kwenye uchaguzi akiwa katika nafasi bora baada ya katiba mpya kuidhinishwa mwaka 2023 iliyomruhusu kugombea muhula mwingine.
'Hali ya utulivu kwa ujumla'
Mwakilishi wa ujumbe wa AU, Bernard Makuza, alipongeza uchaguzi huo, ambao ulijumuisha wa wabunge, serikali za manispaa na mikoa kwa wakati mmoja, kama "hatua chanya kuelekea demokrasia."
Waangalizi wa AU walifuatilia uchaguzi wa mwaka huu katika baadhi ya maeneo matatu kati ya 20 ya nchi hiyo.
Makuza, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Rwanda, alisisitiza kwamba "usalama kwa ujumla" wa nchi uliruhusu upigaji kura ufanyike katika "hali ya utulivu kote."
Alisema vyanzo vya humu nchini viliripoti kwamba mchakato wa uchaguzi umeendelea kwa amani kote nchini, isipokuwa katika maeneo machache ya Haut-Mbomou kusini-mashariki.
Mzozo kusini-mashariki
Mkoa huo unakabiliwa na mgogoro kati ya jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati na makundi ya wapiganaji.
Mnamo 2020, asilimia 50 pekee ya maeneo yaliweza kushiriki katika uchaguzi.
Mchakato wa uchaguzi ulitatizwa pia na jaribio la mapinduzi lililoongozwa na waasi wa CPC.
Makuza aliwatahadharisha wagombea wenye malalamiko watumie njia za kisheria kupinga matokeo. Waangalizi wa AU watatuma taarifa zao kamili kwa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.
Matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa tarehe 5 Januari, wakati Mahakama ya Katiba itatangaza matokeo ya mwisho — ikiwa kutapatikana mshindi katika raundi ya kwanza, basi haitohitaji duru ya pili — tarehe 20 Januari.











