| Swahili
UTURUKI
2 dk kusoma
Uturuki na Armenia zakubaliana kurahisisha utoaji wa viza katika jitihada za kuimarisha uhusiano
Wenye pasipoti za kidiplomasia, za huduma rasmi, na maalum kutoka nchi zote mbili watastahiki kupata e-visa bila malipo, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki.
Uturuki na Armenia zakubaliana kurahisisha utoaji wa viza katika jitihada za kuimarisha uhusiano
Rais wa Uturuki Erdogan akutana na Waziri Mkuu wa Armenia Pashinyan katika mkutano wa kilele wa SCO huko Tianjin, China, Septemba 1, 2025. / / Anadolu Agency
29 Desemba 2025

Uturuki na Armenia zimekubaliana kurahisisha taratibu za utoaji wa visa kwa wenye pasipoti za kidiplomasia, za huduma rasmi za kiserikali, na pasipoti maalum, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesema.

Kuanzia Alhamisi, Januari 1, wenye pasipoti za kidiplomasia, za huduma rasmi za kiserikali, na pasipoti maalum kutoka nchi zote mbili watakuwa na haki ya kupata e-visa bila malipo, wizara hiyo ilisema katika taarifa iliyotolewa Jumatatu.

Wizara hiyo iliongeza kuwa katika muktadha huu, Ankara na Yerevan pia zimethibitisha tena dhamira yao ya kuendeleza mchakato wa kurudisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili bila masharti, kwa lengo la kuimarisha ushusiano.

Hatua hii imekuja baada ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kusema mapema mwezi huu kwamba Uturuki itachukua “hatua kadhaa muhimu” kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2026 kama sehemu ya mchakato unaoendelea wa kuimarisha uhusiano na Armenia.

Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan, alipongeza kauli za Erdogan, akisema kuwa “wakati umefika” wa kuusukuma mbele mchakato wa kurekebisha uhusiano kati ya Ankara na Yerevan.

Baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti, Uturuki ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kutambua uhuru wa Armenia mnamo Desemba 1991.

Hata hivyo, mwaka 1993, Uturuki ilifunga mpaka wake na kukata uhusiano baada ya majeshi ya Armenia kukalia maeneo ya Azerbaijan ndani na karibu na Karabakh. Tangu wakati huo, nchi hizo mbili hazijakuwa na uhusiano wa kidiplomasia wala wa kibiashara.

Mchakato wa kuimarisha uhusiano ulianzishwa baada ya vita vya Karabakh vya mwaka 2020, ambavyo Azerbaijan iliweza kurudisha maeneo yake, na hivyo kuingiza uhusiano kati ya Uturuki na Armenia katika awamu mpya.

 Uturuki imeunganisha juhudi zake za kurekebisha uhusiano na Armenia na maendeleo katika mchakato wa amani, ikionyesha kuwa maridhiano mapana zaidi katika eneo la Caucasus ya Kusini yatawezeshwa na kusainiwa kwa mkataba rasmi wa amani kati ya Baku na Yerevan.

CHANZO:TRT World & Agencies, TRT World and Agencies