| Swahili
MICHEZO
1 dk kusoma
Mechi za kuwania kufuzu AFCON 2027 zinaanza huku kukiwa na utata kuhusu bingwa mtetezi
Jumla ya nchi 48 zimegawanywa katika makundi 12 na kila taifa litacheza mechi sita kuwania kufuzu. Michezo hiyo itaendelea hadi mwezi Machi mwakani.
Mechi za kuwania kufuzu AFCON 2027 zinaanza huku kukiwa na utata kuhusu bingwa mtetezi
PICHA YA MAKTABA: Morocco walipewa ushindi 3-0 kwa fainali ya AFCON kufuatia tukio la Senegal kutoka uwanjani.

Mechi za kuwania kufuzu kwa mashindano ya AFCON zinaanza siku ya Alhamisi wakati timu zikijipanga kwa ajili ya 2027, huku kukiwa na utata kuhusu mshindi wa mashindano yaliyopita.

Nchi 48 zimegawanywa katika makundi 12 na zinaanza mchakato wa kucheza mechi sita hadi mwezi Machi mwakani, watakaomaliza nafasi ya kwanza na ya pili katika makundi tisa watafuzu kwa mashindano ya 2027.

Wenyeji wa mechi hizo za 2027 ni Kenya, Tanzania, na Uganda, ambao pia wanashiriki mechi hizi za kuwania kufuzu ila wao wameshapata nafasi tayari. Katika makundi ambayo wao wanacheza, ni timu moja pekee itakayofuzu kwa michuano hiyo ya timu 24, ambayo yatafanyika kuanzia Juni 19-Julai 17.

Hata hivyo, ikiwa imebaki chini ya mwaka mmoja kwa mechi hizo kuchezwa, bado bara zima linasubiri kujua nani hasa ndiye bingwa mtetezi baada ya fainali iliyochezwa Morocco mwezi Januari.

Kupokonywa taji

Senegal iliwafunga wenyeji katika fainali lakini kwa sababu waliondoka uwanjani kwa dakika 14 kupinga maamuzi, walipokonywa taji hilo na Morocco kutangazwa washindi.

Senegal wamekata rufaa dhidi ya uamuzi wa Shirikisho la Soka barani Afrika na itasikilizwa na Mahakama ya Upatanishi ya Michezo Oktoba 8.

CHANZO:TRT Afrika Swahili