Mkuu wa jeshi la Iran Amir Hatami ameonya kuanza kulipiza kisasi "cha kusikitisha" kwa mauaji ya mkuu wa usalama Ali Larijani katika shambulio la anga la Israel.
"Jibu la Iran kwa mauaji ya katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa litakuwa la maamuzi na la kusikitisha," Hatami alisema katika taarifa yake siku ya Jumatano.
Walinzi wa Jeshi la Mapinduzi, kikosi chenye nguvu cha kijeshi cha Iran ambacho kimejitenga na jeshi, kilisema katika taarifa siku ya Jumatano kwamba kilirusha makombora katikati mwa Israel "kulipiza kisasi cha damu ya shahidi Dk Ali Larijani na masahaba wake".
Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa la Iran hapo awali lilithibitisha kuuawa kwa Larijani, baada ya Israel kusema kuwa ilimuua katika shambulio la anga, ambalo pia liligharimu maisha ya mwanawe na walinzi wake.
Larijani alikuwa kiongozi mashuhuri katika siasa za Iran na alishikilia nyadhifa mbalimbali za juu katika kipindi cha miongo minne iliyopita, ikijumuisha vyombo vya habari vya serikali, taasisi za usalama, na bunge.
Alizaliwa tarehe 3 Juni 1957 huko Najaf, Iraq. Larijani alihitimu shahada ya kwanza katika Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Sharif cha Teknolojia na alipata shahada za uzamili na udaktari katika falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Tehran.





