Akizungumza katika ujumbe wa Mwaka Mpya, Fidan alisema kuwa Uturuki itaendelea kuongoza juhudi za kuleta amani, utulivu na ustawi mwaka 2026, huku ikiimarisha diplomasia ya uhusiano na pande nyingi na kutekeleza wajibu wake wa kibinadamu.
Katika taarifa aliyoichapisha kwenye mitandao ya kijamii ya NSosyal na X siku ya Jumatano, Fidan alisema kuwa katika mwaka uliopita Uturuki imekubalika kama mshirika anayeaminika na kituo muhimu cha kutatua migogoro katika maeneo mbalimbali duniani, kuanzia Gaza na Ukraine hadi Kusini mwa Caucasus na Pembe ya Afrika.
Alisema kuwa Uturuki, chini ya uongozi wa Rais Recep Tayyip Erdogan, imefuata sera ya mambo ya nje yenye mwelekeo mpana, yenye msukumo, uwiano na uhalisia, kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa na kutetea kile alichokiita misimamo ya haki ya Uturuki.
“Tulifanya kazi bila kuchoka kulinda maslahi yetu ya kitaifa, kutetea haki zetu, na kufanya ushawishi wa Uturuki utambulike,” alisema Fidan.
“Mnamo mwaka 2026, kwa azma ileile, tutaendeleaza juhudi za amani, utulivu na ustawi, kuchangia diplomasia ya pande nyingi, na kutimiza majukumu yetu katika masuala ya kibinadamu.”
Fidan pia aliwatakia heri ya Mwaka Mpya raia wa Uturuki walioko nchini na nje ya nchi, akitarajia mwaka 2026 ulete amani na mazuri kwa Uturuki, raia wake, na watu wote kwa ujumla.



















