ULIMWENGU
5 dk kusoma
Namna Pakistan na Afghanistan inayoongozwa na Taliban ilivyopatanishwa tena na China
Baada ya miaka kadhaa ya makabiliano mpakani na kutoaminiana, Pakistan na Afghanistan wameanzisha ushirikiano wa kidiplomasia, huku China ikisaidia kimya kimya kutuliza hali, lakini bado kuna changamoto kubwa.
Namna Pakistan na Afghanistan inayoongozwa na Taliban ilivyopatanishwa tena na China
Hatua za tahadhari katika kuimarisha tena uhusiano wa nchi mbili (AP). / AP
17 Juni 2025

Baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, Pakistan na viongozi wa Taliban nchini Afghanistan wamerudi tena kwenye meza ya majadiliano, wakizungumzia namna ya kusuluhisha matatizo.

Nchi hizo mbili zimechukua hatua ya kuweka sawa uhusiano, ishara kamili ikiwa uteuzi wa hivi majuzi wa mabalozi wa mataifa yao.

China inasemekana kuwa na jukumu kubwa zaidi katika hili, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tatu jijini Beijing 21 Mei. Mkutano huo ulisaidia kutuliza hali kati ya Pakistan na Afghanistan.

Wanadiplomasia nchini Pakistan wanaona kama ni “hatua muhimu”. Pamoja na kuwa haijautambua kikamilifu utawala wa Taliban nchini Afghanistan kama wa halali, kwa mbali inawakubali kama viongozi wa taifa hilo.  

Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan Ishaq Dar, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje, akiwa Hong Kong alitangaza uteuzi wa balozi wao wa nchini Afghanistan.

Hii imeashiria mabadiliko ya hapo awali ambapo Pakistan ingesubiri mataifa ya magharibi yakiongozwa na Marekani kuwapa ruhusa ya kufanya hivyo.

Pamoja na kuwa hawajatambuliwa rasmi, hatua hii inaonesha mabadiliko muhimu ya kisera, yale ambayo yanaendana na kukubaliwa kwa serikali ya Taliban katika kanda. 

China inaongoza, wengine wanafuata

China, ambayo iliimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Taliban ya Afghanistan 2023, tayari imefanya uwekezaji mkubwa, hasa katika sekta ya madini nchini Afghanistan.

Sasa China ina ushawishi mkubwa nchini humo kwa kuibuka kuwa mdau muhimu katika nchi hiyo ambayo haina bahari baada ya kuondoka kwa vikosi vya NATO vilivyokuwa vinaongozwa na Marekani.

China pia imefanya Afghanistan kuwa sehemu ya mpango wa ushoroba wa uchumi wa China na Pakistan (CPEC), ambao ndiyo mradi wao mkubwa wa ‘‘Belt and Road Initiative’’ (BRI). Hii ni sababu nyingine kwa Afghanistan na Pakistan kutatua matatizo yao na kuangazia zaidi suala la uchumi, biashara na fursa za uwekezaji. 

Wakati huohuo, mabadiliko ya kikanda yanaendelea. Urusi na Kazakhstan wameshawaondoa Taliban katika orodha ya magaidi, na vyanzo vya kidiplomasia vinasema kuwa Tajikistan inatarajiwa kufanya hivyo pia.  

Uzbekistan tayari imeanzisha njia ya uchumi huru katika mpaka wake na Afghanistan, ambapo raia wa Afghanistan wanaruhusiwa kuingia nchini humo kwa muda wa wiki mbili bila kulipia viza.  

Kwa Pakistan, hili lina umuhimu mkubwa. Kuimarishwa kwa usalama nchini Afghanistan hatimae kunaweza kubadlisha biashara ya nchi hiyo ya Asia ya kati kukamilisha lengo lake la mahitaji ya nishati kutoka kwa Turkmenistan, Tajikistan na Kyrgyzstan. Ndoto hiyo pia inajumuisha ujenzi wa barabara, kuunganisha Uzbekistan, Afghanistan na Pakistan.

Historia  

Hata hivyo, historia na siasa za dunia inafanya jukumu la kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati ya majirani wawili kuwa gumu, kama siyo kutowezekana.

Siyo muda mrefu uliopita, Pakistan na Afghanistan walikuwa wanashambuliana maeneo ya mipakani. Pakistan imekuwa ikiilaumu Taliban kwa kuwapa makazi makundi ya wapiganaji dhidi ya Pakistan, ikiwemo Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP), tangu waliporudi madarakani Agosti 2021.

Pakistan inalaumu Afghanistan kwa kuruhusu makundi yanayotaka kujitenga kutumia ardhi yake kufanya mashambulizi katika mkoa uliokumbwa na vurugu wa kusini magharibi wa Balochistan. Makundi ya wapiganaji, ikiwemo Jeshi la Ukombozi la Balochistan (BLA) na TTP, pia yanashirikiana kufanya mashambulizi ya kigaidi, ambalo ni jambo lisilokuwa la kawaida.   

Afghanistan inakanusha madai hayo na kutaka Pakistan itafute suluhu ya changamoto zake za ugaidi ndani ya nchi.  

Wakati mashambulizi ya kigaidi yalipoongezeka ndani ya Pakistan, walianza kuchukua hatua kali, ikiwemo pamoja na kuwarudisha Afghanistan wakimbizi ambao hawakuwa na hadhi rasmi.

Tangu Oktoba 2023, raia wa Afghanistan zaidi ya 850,000 wamerudishwa.

Pakistan bado ni mwenyeji wa zaidi ya wakimbizi wa Afghanistan milioni tatu. Inajumuisha watu milioni 1.3 ambao wana vitambulisho vya ‘ushahidi wa usajili’ na 800,000 au zaidi wenye kadi za uraia wa Afghanistan, lakini karibu milioni moja wanaishi kwa njia ya haramu bila nyaraka zozote.

Pakistan imekuwa ikiwachukua wakimbizi wa Afghanistan tangu 1979, wakati vikosi vya uliokuwa muungano wa Sovieti wakati vilivyopoingia Afghanistan. Hata hivyo, kuwafukuza wakimbizi ni sehemu moja ya changamoto walizonazo.

Pakistan pia inajenga uzio wa kilomita 2,640 katika mpaka wao na Afghanistan na kuanzisha utaratibu wa kupata viza, ikiwa ni tofauti kubwa na zamani wakati raia wa Afghanistan walikuwa wanavuka bila kuhitajika kuonesha nyaraka nyingi.

Vikwazo hivi pia vinatatiza kuvuka mipaka kwa watu wa jamii zenye utamaduni mmoja na uhusiano wa kiuchumi. Taliban, ambayo kwa sehemu kubwa ni watu wa Pashtun wenyewe, wanaona hatua hizi kama zinazoleta uhasama.

Kukatishwa tamaa kwa Pakistan

Pakistan ilitarajia kuwa kurudi kwa Taliban, washirika wake wa muda mrefu wakati Marekani ilipokuwa imekalia nchi hiyo, kungehakikisha kuwepo kwa serikali yenye urafiki ya Afghanistan, tofauti na viongozi waliopita ambao walikuwa na ukaribu zaidi na India.

Wakati wa vikosi vya NATO vilivyoongozwa na Marekani vilipokalia Afghanistan, serikali ya Hamid Karzai na Ashraf Ghani ziliendelea kuwa na uhusiano wa karibu na India, na kuwa na ubalozi katika miji ya Jalalabad na Kandahar, maeneo ambayo Pakistan inalaumu kwa kutumika kwa ujasusi na kufadhili ugaidi – madai ambayo India inakanusha.

Uongozi wa Taliban nchini Afghanistan

Kwa Pakistan, suala la msingi zaidi ni lile la ugaidi. Lakini kuwashurutisha Taliban kukabiliana na TTP si rahisi. Viongozi na wapiganaji wao kutoka kwa makundi yote mawili walipata mafunzo yao nchini Pakistan na itikadi yao ni sawa.

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya Pakistan wanasema kuwa Pakistan inatakiwa isitizame Afghanistan kama wenyeji wa kundi la wapiganaji la TTP. Kinachotakiwa ni kujadiliana nao katika masuala ya – kiuchumi, kidiplomasia, na kitamaduni. 

Kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kwa uhakika ni hatua nzuri sana. Pakistan na Afghanistan wako njia panda: waendelee na kutoaminiana au wakubaliane kuungana kidiplomasia kwa kuzingatia maslahi ya kiuchumi na ya kiusalama. 

Kuanzisha tena uhusiano wa kuwepo kwa mabalozi huenda ikawa ni hatua ya mwanzo, lakini ni fursa muhimu. Mataifa yote mawili na kanda nzima itafaidika iwapo wataungana pamoja katika hili.

CHANZO:TRT World