Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume wakisaini Hati za Makubaliano ya Muungano, Tarehe 22 Aprili, 1964 Zanzibar. ./Picha: Ofisi ya Makamu wa Rais/Muungano-Tanzania 

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Tanzania inaingia kwenye shamrashamra kubwa wakati itapokuwa ikiadhimisha miaka 60 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Tayari, viongozi mashuhuri wakiwemo Rasi wa Kenya William Ruto na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamethibitishwa kushiriki katika sherehe hizo zitakazofanyika Aprili 26, 2024 katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Wengine ni Hakainde Hichilema wa Zambia, Azali Assoumani wa Comoro, Nangolo Mbumba wa Namibia na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.

Pia wapo Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Klaus Chilima, Jessica Alupo wa Uganda na Waziri Mkuu wa Msumbiji Adriano Maleiane.

Taifa la Tanzania, au Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilizaliwa baada ya kuunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, mnamo Aprili 26, 1964.

Ishara ya kuchanganya udongo

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964./Picha: Ofisi ya Makamu wa Rais/Muungano-Tanzania

Tukio la utiaji sahihi wa Hati za Muungano la tarehe 22 Aprili, 1964 lilikuwa ni ndoto ya waasisi wa Muungano iliyotafsiriwa kwa vitendo kwa kuimarisha rasmi uhusiano huo kwa mujibu wa Mapatano ya Muungano. Mapatano hayo yalisainiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umejengeka kutokana na historia ya uhusiano wa udugu wa damu, harakati za pamoja na ushirikiano wa vyama vya ukombozi vya Tanganyika na Zanzibar katika kupigania uhuru.

Upekee wake

Pamoja na Hati ya Makubaliano ya Muungano kusainiwa tarehe 22 Aprili, 1964 zipo sababu za kihistoria na kimahusiano zilizochochea nchi hizi kuungana na Muungano huo kushamiri na kudumu. Sababu hizo ni pamoja na ujirani wa karibu; urafiki na udugu wa damu wa miaka mingi; lugha ya pamoja ya mawasiliano – Kiswahili; shughuli za pamoja za kiuchumi – uvuvi, kilimo na biashara; uzoefu wa pamoja vipindi vya utumwa na ukoloni; na mahusiano ya karibu ya kisiasa katika kupigania uhuru wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Sababu hizi ndizo zinazoufanya Muungano wa nchi hizi mbili kuwa wa kipekee, na ni sababu ambazo hazina budi kuzingatiwa na wadau, watafiti na waandishi wa historia wanapolitalii suala hili adhimu la Muungano huo. Bila kufanya hivyo, chimbuko la Muungano wa Tanzania halionekani bayana na upekee wa Muungano huo haujitokezi waziwazi.

Juhudi za kutosha zimefanywa na Serikali zote mbili – Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa wanafunzi wengi wa ngazi mbalimbali pamoja na wananchi kwa ujumla wanapata taarifa sahihi kuhusu historia, changamoto na mafanikio makubwa ya Muungano wa Tanzania ambao umebaki kuwa Muungano pekee barani Afrika uliodumu na kushamiri kwa zaidi ya nusu karne na kuendelea kuyaishi malengo ya Umajumui wa Afrika.

Muungano kati ya Tangayika na Zanzibar umedumu kutokana na mizizi yake kujikita kwa wadau wakuu wa Muungano ambao ni wananchi na umakini na usikivu wa serikali zote mbili, yaani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Sio ajabu kuona vikao vya pamoja vya kujadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza kwa kuzingatia misingi ya umoja na mshikamano, umeimarisha na kudumisha Muungano kwa kiasi kikubwa.

Mwalimu Julius K. Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume wakipungia wananchi wakati wa sherehe za Muungano zilizofanyika Dar es Salaam tarehe 26 Aprili, 1964./Picha:Ofisi ya Makamu wa Rais/Muungano-Tanzania

Ndani ya miaka ya 60, muungano huo umeshuhudia mafanikio makubwa ya kujivunia ukiwa ndio muungano pekee uliodumu kati ya majaribio kadhaa ya aina hiyo barani Afrika.

Muungano huo umeendelea kuimarika kwa amani, utulivu pamoja na ulinzi na usalama ndani ya nchi na kwenye mipaka ya nchi hiyo.

Ni kupitia muungano huu, raia kutoka Tanzania bara wamekuwa na familia katika upande wa pili wa muungano.

Hata katika muundo wa kiserikali, zipo baadhi ya Wizara za kimuungano, kupitia mpangilio huu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sehemu ya Pili, Ibara ya 47, Ibara ndogo ya kwanza (1): “Kutakuwa na Makamu wa Rais ambaye atakuwa ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais kuhusu mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa jumla…”

“Ibara hiyo hiyo ya 47, Ibara ndogo ya tatu (3): Mtu atateuliwa kugombea kiti cha Makamuwa Rais kwa kufuata kanuni kwamba endapo Rais wa Jamhuru ya Muungano atattoka sehemu moja ya Muungano basi Makamu wa Rais atakuwa ni mtu anayetoka sehemu ya pili ya Muungano.”

Tanzania ilipoundwa Aprili 26, 1964 Mwalimu Julius Nyerere alikuwa Rais wa Kwanza na Makamu wake alikuwa Sheikh Abeid Amani Karume na Rashid Mfaume Kawawa alikuwa Makamu wa Poli wa Rais.

Yaani Rais akitoka Tanzania Bara, Makamu wa Kwanza wa Rais atatoka Tanzania Visiwani na Makamu wa Pili atatoka Tanzania Bara na kinyume chake kama Rais atakuwa ametoka Visiwani.

Kwa mfano, Rais wa sasa wa Tanzania ni mzaliwa wa Zanzibar. Aliwahi kuhudumu kama mbunge wa Jimbo la Makunduchi katika Bunge la Muungano, kati ya 2000 mpaka 2010.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Samia alichaguliwa kama Makamu wa Rais na baadaye Rais kufuatia kifo cha ghafla cha John Pombe Magufuli, Machi 2021.

Hata hivyo, ni vyema kuyafahamu baadhi ya mambo ambayo ni ya kimuungano. Yanajumuisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Suala la Ulinzi na Usalama na Jeshi la Polisi.

Mengine ni Sheria ya Uraia Namba 6 ya mwaka 1995, Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na Simu.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akimkaribisha Sheikh Abeid Amani Karume katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam wakati wa sherehe za  Muungano tarehe 26 Aprili, 1964./Picha: Ofisi ya Makamu wa Rais/Muungano-Tanzania

Licha ya kuwa na bendera yake na wimbo wake wa Taifa, Zanzibar hutumia nyenzo hizo mbili wakati wa masuala yanayohusu visiwa hivyo tu, kwa mfano wakati wa sherehe za mapinduzi na sio wakati wa masuala ya Muungano.

TRT Afrika