Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Hussein Bashe./Picha: TRT Afrika

Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe amesisitiza kuwa Tanzania haihusiki na usambazwaji wa mbolea nchini Kenya.

Kupitia ukurasa wake wa X, Waziri Bashe amepinga vikali madai ya wakili maarufu nchini Kenya, Ahmednassir Abdullahi kuwa Tanzania ilikuwa chanzo cha mbolea hizo feki, na kuhoji kama ulikuwa ni 'ubishi wa kawaida na kejeli' baina ya majirani hao wawili kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Kulingana na Bashe, Tanzania haihusiki na kashfa ya mbolea feki iliyoikumba nchi ya Kenya, na kuongeza kuwa nchi hiyo haijawahi kusafirisha bidhaa feki nchini Kenya, ikiwemo mbolea.

Katika majibizano hayo, Bashe alimtaka Ahmednassir kuacha kuiingiza wala kuihusisha Tanzania na mambo yasiyokuwa na maana.

"Kama mna mambo yenu, nawashauri myamalize, muache kutuhusisha na hayo mambo, " ameandika Bashe.

Awali, wakili huyo maarufu kutoka Kenya alidai kuwa ana fahamu mahali inapotengenezwa mbolea hiyo feki, na kudai kuwa ni Tanzania.

TRT Afrika