| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Afya ya Besigye yazorota, chama chake chasema
Afya ya kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda aliyefungwa gerezani, Kizza Besigye, imedhoofika, chama chake kilisema siku ya Jumanne, baada ya kupelekwa usiku katika kituo cha afya kilichopo katika mji mkuu, Kampala.
Afya ya Besigye yazorota, chama chake chasema
Besigye aligombea urais mara ya mwisho mwaka 2016. / / AP
20 Januari 2026

Chama cha upinzani nchini Uganda cha People’s Front for Freedom kilisema katika taarifa kwamba afya ya Kizza Besigye “iko katika hali mbaya na inaendelea kudhoofika,” kikitaka aruhusiwe kukaguliwa na madaktari wake binafsi pamoja na familia yake.

Haya yanajiri baada ya kupelekwa katika kituo cha afya kilichopo katika mji mkuu, Kampala usiku.

Besigye, mwanasiasa mkongwe ambaye alikuwa kiongozi maarufu zaidi wa upinzani nchini Uganda kabla ya kupanda kwa umaarufu wa Bobi Wine, anazuiliwa katika gereza lenye ulinzi mkali jijini Kampala. Anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya uhaini, ambayo anasema yana malengo ya kisiasa.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba mtu aliyejitolea kwa ajili ya afya na uhuru wa wengine ananyimwa haki yake ya kupata matibabu,” ilisema taarifa ya People’s Front for Freedom.

“Tunaitaka serikali na mamlaka za magereza kuwajibika kikamilifu kwa afya yake.”

Frank Baine, msemaji wa Idara ya magereza wa Uganda, alikanusha madai ya kudhoofika kwa afya ya Besigye. “Ilikuwa ni uangalizi wa kawaida tu,” alisema kuhusu safari ya Besigye ya kupelekwa kwa daktari usiku. “Asubuhi ya leo alikuwa akifanya mazoezi yake kama kawaida.”

Besigye aligombea urais mara ya mwisho mwaka 2016. Baadaye alisema kuwa uchaguzi ni kupoteza muda katika nchi inayoongozwa na kiongozi wa kiimla ambaye mamlaka yake yanategemea majeshi ya usalama.

Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, alitangazwa Jumamosi kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika wiki iliyopita.

Kulingana na matokeo rasmi, Museveni alipata asilimia 71.6 ya kura huku mpinzani wake wa karibu zaidi, Bobi Wine, akipata asilimia 24.7.

Wine alikataa matokeo hayo na kuyataja kuwa ya kighushi.

CHANZO:AP