AFRIKA
2 DK KUSOMA
Rais Samia wa Tanzania akutana na Rais Novak wa Hungary
Marais wanawake wa Tanzania na Hungary walikutana Ikulu Tanzania katika tukio la kihistoria kwa sababu wote ni marais wa kwanza wanawake wa nchi zao.
Rais Samia wa Tanzania akutana na Rais Novak wa Hungary
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mgeni wake Rais wa Hungary Mhe. Katalin Novák mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe18 Julai, 2023 | Picha: Ikulu Tanzania / Others
19 Julai 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema licha ya kuendeleza majadiliano ya kidiplomasia, Tanzania na Hungary wamebainisha maeneo mapya ya ushirikiano

Kupitia taarifa kutoka Ikulu ya Tanzania maeneo hayo ya ushirikiano ni pamoja na biashara na uwekezaji, elimu, utalii na pia uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake.

Rais Samia amesema hayo tarehe 18 Julai akiwa na mgeni wake Rais wa Hungary, Mhe. Katalin Novák aliyepo Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku 3 wakati wakizungumza na vyombo vya habari.

Wakati huo huo, Rais Samia ametoa wito kwa raia wa Hungary kuja kuwekeza kwenye sekta ya utalii nchini Tanzania.

Rais Samia amesema idadi kubwa zaidi ya watalii wapatao 7,188 kutoka Hungary wametembelea Tanzania kwa mwaka 2022 na anatarajia kuwa baada ya ziara ya Rais Novák idadi hiyo itaongezeka.

Kwa upande wake Rais Novák ametoa mwaliko kwa Rais Samia kushiriki katika mkutano wa masuala ya idadi ya watu utakaofanyika mwezi Septemba na mkutano wa viongozi wanawake utakaofanyika mwakani nchini Hungary.

Hungary na Tanzania zimetia saini Hati ya Makubaliano kuhusu ushirikiano wa ufadhili wa masomo ya Elimu ya Juu (Scholarship) utakaotolewa baina ya nchi hizo mbili.

CHANZO:TRT Afrika