AFRIKA
2 DK KUSOMA
Kagame, Tshisekedi kukutana Dar es Salaam kwa suala la DRC Mashariki
Uthibitisho wa wawili hao kukutana umetolewa na Rais William Ruto wa Kenya, Februari 3, 2025.
Kagame, Tshisekedi kukutana Dar es Salaam kwa suala la DRC Mashariki
Viongozi hao wawili wanatarajia kukutana katika Mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendelea Kusini mwa Afrika (SADC)./Picha: TRT Afrika / Others
3 Februari 2025

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Paul Kagame wa Rwanda, wanatarajia kukutana jijini Dar es Salaam, Februari 8, 2025 kujadili mustakabali wa hali ya usalama katika eneo la Mashariki mwa DRC.

Taarifa iliyotolewa na Rais wa Kenya William Ruto, wawili hao watakutana katika mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), baada ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kuridhia nchi yake kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Hatua hiyo inafuatia makubaliano kati ya mwenyekiti wa SADC Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Rais William Ruto wa Kenya, ambaye pia ni mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya EAC.

“Rais Samia Suluhu Hassan amekubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao unalenga kutafuta suluhu ya mgogoro wa Mashariki mwa DRC," alisema Rais Ruto.

Kulingana na Rais Ruto, wawili hao wamethibitisha uwepo wao kwenye mkutano huo wa pamoja ambao utatanguliwa na mkutano wa mawaziri siku ya Ijumaa, kabla ya Wakuu wa EAC na SADC hawajakutana siku ya Februari 8, 2025.

Rais Ruto pia amesema kuwa amewashirikisha jambo hilo Marais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Yoweri Museveni wa Uganda na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika