Adeniyi Mobolaji Kayode, mwenye umri wa miaka 46, alishtakiwa kwa kuendesha gari kwa uzembe na kwa hatari, polisi katika jimbo la Ogun, kusini-magharibi mwa Nigeria, walisema Ijumaa.
Dereva huyo alikuwa akiendesha gari lililombeba bondia Anthony Joshua pamoja na marafiki zake wawili, Latif Ayodele na Sina Ghami, kwenye barabara kuu inayounganisha Lagos na Ibadan, kusini-magharibi mwa Nigeria, wakati gari aina ya Lexus SUV walilokuwa wakisafiria lilipogonga lori lililokuwa limesimama kando ya barabara siku ya Jumatatu.
“Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana ya naira milioni tano (sawa na dola 3,480 za Marekani) akiwa na wadhamini wawili. Aliwekwa rumande akisubiri kutimiza masharti ya dhamana,” alisema msemaji wa polisi Oluseyi Babaseyi alipokuwa akizungumza na shirika la habari la AFP.
Uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi kupita kiasi, aidha tairi la gari hilo pia lilipasuka kabla ya ajali kutokea, kulingana na Wakala wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria za Trafiki (TRACE) katika jimbo la Ogun, ambako ajali hiyo ilitokea.
Maafisa wa serikali ya jimbo hilo walisema Jumatano kuwa Joshua aliruhusiwa kutoka hospitalini.
Baada ya kuondoka hospitalini, Joshua na mama yake walienda kutoa heshima zao katika kituo cha kuhifadhia maiti ambako miili ya marafiki zake ilikuwa “ikiandaliwa kwa ajili ya kurejeshwa makwao,” maafisa hao waliongeza.



















