Raia wa Sudan Kusini huenda wakaendelea kuishi na kufanya kazi nchini Marekani kisheria, huku jaji wa shirikisho siku ya Jumanne akiendelea kutathmini kama hatua ya Rais Donald Trump ya kufuta hadhi ya ulinzi wa muda kwa wahamiaji kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilikuwa kinyume cha sheria.
Kufutwa kwa hadhi hiyo kulipangwa kuanza kutekelezwa tarehe 6 Januari 2026. Kufikia wakati huo, takribani raia 300 wa Sudan Kusini waliokuwa wakiishi na kufanya kazi Marekani chini ya mpango huo — au waliokuwa na maombi yanayoendelea — wangeweza kufukuzwa nchini humo.
Mashirika ya haki za kiraia yaliishtaki Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani (DHS) mwishoni mwa Desemba, yakidai kuwa mabadiliko hayo yalikiuka taratibu za kisheria za utawala na yalikuwa kinyume na Katiba kwa sababu yalilenga “kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wahamiaji wasio wazungu na wasio wa Ulaya nchini Marekani” kwa misingi ya rangi.
Amri ya mahakama iliyotolewa na Jaji wa Wilaya ya Marekani Angel Kelley huko Massachusetts imeizuia kwa muda serikali ya shirikisho kuanza kuwafukuza wahamiaji hadi uamuzi wa mwisho utakapofanyika.
‘Madhara makubwa yenye pana’
“Matokeo haya makubwa na yenye athari pana si tu kwamba yanastahili, bali yanahitaji uchunguzi kamili na wa kina wa hoja za kisheria na Mahakama,” Kelley aliandika, akiongeza kuwa mabadiliko hayo yanaweza kusababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa kwa wahamiaji kutoka Afrika Mashariki.
DHS ilikosoa vikali uamuzi huo katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne.
“Huu ni uamuzi mwingine wa kiholela na wa kiuanaharakati kutoka kwa mahakama ya shirikisho, ambayo inaendelea kunyakua mamlaka ya kikatiba ya Rais. Chini ya utawala uliopita, hadhi ya ulinzi wa muda ilitumiwa vibaya kuruhusu magaidi wakatili, wahalifu na vitisho vya usalama wa taifa kuingia nchini,” aliandika Tricia McLaughlin, Msaidizi wa Katibu wa DHS.
Hadhi ya ulinzi wa muda hutolewa kwa raia wa kigeni kutoka nchi zilizoathiriwa vibaya na vita au majanga ya asili. Waombaji wanaofanikiwa lazima tayari wawe wanaishi Marekani na wapitie uchunguzi mkali wa historia na usalama unaofanywa na DHS.
Bila kutoa ushahidi, McLaughlin alidai kuwa kuna “amani nchini Sudan Kusini” na akaeleza kuwa kuna “jitihada za kuhakikisha raia wanaorejea wanaunganishwa salama na jamii, pamoja na kuboreshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia.”
Raia wa Sudan Kusini walianza kustahili hadhi ya ulinzi wa muda mwaka 2011. Miaka ya migogoro imeifanya nchi hiyo kutegemea sana misaada ya kibinadamu, ambayo imeathiriwa pakubwa na upunguzaji mkubwa wa misaada ya kigeni chini ya utawala wa Trump.
Msako mkali wa Trump dhidi ya wahamiaji
Utawala wa Trump umejaribu kuondoa aina mbalimbali za ulinzi uliowawezesha wahamiaji kubaki Marekani na kufanya kazi kisheria. Hatua hizo ni pamoja na kusitisha hadhi ya ulinzi wa muda kwa mamia ya maelfu ya raia wa Venezuela na Haiti waliokuwa wamepewa ulinzi huo chini ya Rais Joe Biden.
Hadhi ya ulinzi kwa wahamiaji kutoka Ethiopia, Cameroon, Afghanistan, Nepal, Myanmar (Burma), Syria, Nicaragua na Honduras pia iko hatarini.













