Mgombea wa CCM Tanzania: Safari ya kisiasa ya Rais Samia Suluhu Hassan
AFRIKA
2 dk kusoma
Mgombea wa CCM Tanzania: Safari ya kisiasa ya Rais Samia Suluhu HassanChama tawala nchini Tanzania CCM kiko mbioni kutetea nafasi ya uongozi wake.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania / Others
2 Septemba 2025

Bendera ya Chama cha Mapinduzi, katika uchaguzi wa Oktoba 29, inapeperushwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akishirikiana na mgombea wake mwenza Emmanuel John Nchimbi.

 Rais Samia aliingia kwenye uongozi wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania mwezi Machi 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli.

 Hii itakuwa mara yake ya kwanza kuingia katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya urais, licha ya kuwepo katika siasa kwa muda mrefu.

Samia Suluhu Hassan, alizaliwa miaka 65 iliyopita Zanzibar, na amewahi kuwa waziri katika serikali ya visiwani huko kuanzia mwaka 2000 hadi 2010.

Kati ya 2010 – 2015 alikuwa Waziri wa Nchi, Masuala ya Muungano.

Vile vile, alikuwa Makamu Mwenyekiti katika Bunge la Katiba ambalo ndilo lililosimamia uliokuwa mchakato wa kuandaa rasimu ya katiba mpya, ambayo utekelezaji wake haukukamilika.

Mwaka 2015, pasina kutarajia, alipendekezwa kuwa mgombea mwenza wa hayati John Pombe Magufuli.

Hatua ambayo, ilimfanya aingie katika historia ya chama hicho kikongwe kuweka mgombea mwenza mwanamke. Hivyo baada ya uchaguzi huo, Samia aliingia katika historia ya Tanzania ya kuwa makamu wa kwanza wa rais mwanamke.

Wawili hao, waliingia tena katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa 2020 na kuibuka kidedea

Lakini kifo cha Magufuli kilibadilisha kabisa taswira ya utawala wa nchi kwani, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, nafasi ya Magufuli ilitakiwa kuchukuliwa na makamu wake.

Machi 19, 2021, Samia alikula kiapo mbele ya Jaji Mkuu cha kuliongoza taifa hilo kwa uadilifu na utii wa sheria.

Rais Samia ana Shahada ya Uzamili katika Maendeleo ya Jamii

 Mapema mwaka huu, Rais Samia bila kupingwa aliteuliwa na chama kugombea nafasi ya urais. Hata hivyo, baadhi walionekana kupinga uteuzi huo wa chama kwa madai kwamba, umekiuka demokrasia ya chama.

Rais Samia Suluhu Hassan anakiongoza chama chake kuwania kurudi madarakani, huku upinzani ukiwa mbioni kutaka kukiondoa uongozini chama ambacho kimekuwa sehemu ya siasa na maisha ya taifa hilo la Afrika Mashariki lenye watu zaidi ya milioni 67 kwa miongo kadhaa.

Ingawa chama kikuu cha upinzani Chadema hakishiriki uchaguzi wa mwaka huu, Rais Samia atashindana na wagombea urais kutoka vyama vya upinzani, ikiwemo CHAUMMA na vyenginevyo.