Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania INEC imesema katika taarifa yake ya tarehe 15 Septemba kwamba, imeondoa jina la mgombea urais wa ACT Wazalendo Luhaga Mpina katika orodha ya wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo.
INEC imesema, awali ilipokea mapingamizi manne ambapo moja kati ya hayo ndilo lililokubaliwa na mengine matatu yamekataliwa.
"Tume imekubali pingamizi lililowasilishwa na Ndugu Hamza Saidi Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo," imesema taarifa ya Tume iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima R.K.
Pingamizi hili linakuja siku chache tu baada ya Mahakama Kuu nchini humo kusikiliza kesi ya hapo awali ambapo Mpina alikosa uteuzi wa Tume ya Uchaguzi kufuatia pingamizi la Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu uteuzi wake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ACT Wazalendo, ni kwamba Mpina amerudisha majibu ya mapingamizi aliyowekewa dhidi yake kwa Tume.
"Leo Septemba 14, 2025, Mgombea Urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Ndugu Luhaga Joelson Mpina amerejesha majibu ya mapingamizi kwa Tume ya Uchauguzi aliyowekewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mgombea Urais wa AAFP na Mgombea Urais wa NRA," imesema ACT Walezalendo.
Kuenguliwa huku kunafanyika licha ya amri ya Mahakama Kuu kuitaka Tume Huru ya Uchaguzi kutopokea amri kutoka taasisi au ofisi yoyote ya serikali kwa sababu Tume hiyo ni Huru kama lilivyo jina lake.