Polisi nchini Nigeria wamethibitisha kuwa watu wengi walitekwa nyara katika jimbo la kaskazini kati la jimbo, kubadilisha taarifa waliokuwa wametoa awali ya kukanusha na kusababisha kushtumiwa.
Katika taarifa iliotolewa siku ya Jumanne na msemaji wa polisi Benjamin Hundeyin, inasema polisi walikiri “kutokea” kwa shambulio hilo na watu wengi walitekwa nyara, siku moja baada ya kukanusha taarifa za utekaji kutoka katika kanisa eneo la Kurmin Wali, huko Kajuru.
Vyombo vya habari vya eneo hilo vilieleza kuwa magaidi, walivamia eneo hilo siku ya Jumapili 18 Januari, na kuwateka watu zaidi ya 160 wakati wa ibada kanisani.
Chama cha Wakristo nchini Nigeria (CAN) kililiambia gazeti la Premium Times kuwa watu 172 awali walisemekana kuwa wametekwa, tisa kati yao baadae walikimbia, na wengine waliobaki walipelekwa katika msitu wa karibu.
Chama cha Christian Solidarity Worldwide Nigeria (CSW-N) kilisema katika taarifa siku ya Jumanne kuwa walishambulia wakati ibadi ikiwa inaendelea.
Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na msemaji Reuben Buhari, iliorodhesha makanisa yaliyoshambuliwa kuwa ni Evangelical Church Winning All (ECWA), Albarka Cherubim na Seraphim 1, na Haske Cherubim na Seraphim 2.













