Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa Marekani haikuwa na taarifa kuhusu shambulizi la Israel katika eneo la gesi la Iran South Pars, na kusema Israel haitashambulia tena labda Iran ilipize, huku akitishia kwamba mashambulizi yoyote dhidi ya miundombinu ya gesi ya Qatar yataifanya Marekani kuharibu miundombinu ya Iran.
"Marekani haikuwa na taarifa yoyote kuhusu shambulio hilo (katika eneo la South Pars), na Qatar, haikuhusika kwa namna yoyote, na pia haikuwa na taarifa kwamba shambulio hilo lingetokea," aliandika Trump katika mtandao wa Truth Social.
Madai yake yanaonekana kukinzana na taarifa za awali kwamba Marekani ilikuwa na taarifa ya shambulio hili mapema lakini haikushiriki.
Amesema Iran imeipiga "bila sababu na kwa uonevu" sehemu ya miundombinu ya gesi ya Qatar katika mji wa viwanda wa Ras Laffan.
Trump alilielezea shambulio hilo la Israel katika eneo la South Pars kwamba "Israel ilishambulia," miundombinu hiyo kwa "hasira," na kusema "ni sehemu ndogo tu" iliyoshambuliwa.
Alitahadharisha kwamba iwapo miundombinu ya gesi ya Qatar itashambuliwa tena, basi Marekani "itashambulia eneo lote la Gesi la South Pars" kwa kushirikiana au bila kushirikiana na Israel katika kiwango ambacho "hakijawahi kutokea."
Amesema hataki kutoa ruhusa ya uharibifu huo ikizingatiwa madhara yake kwa mustakbali wa Iran lakini hatasita kuchukua hatua.
Shambulio la anga la Israel lililenga sehemu ya Iran ya uzalishaji wa gesi South Pars Jumatano, na kuathiri uzalishaji katika mitambo miwili ya kuchakata gesi.
Qatar imeripoti mashambulizi mawili ya makombora katika Mji wa Viwanda wa Ras Laffan, Jumatano na Alhamisi.
Kwa kujibu, Qatar imewataka wanajeshi wa Iran na wafanyakazi wa usalama katika ubalozi wake pamoja na watumishi wengine kuondoka nchini humo.






