Yaliyojiri 2025: Siasa za Kenya baada ya kifo cha Raila Odinga
AFRIKA
2 dk kusoma
Yaliyojiri 2025: Siasa za Kenya baada ya kifo cha Raila OdingaWataalamu wa masuala ya kisiasa nchini Kenya wanasema Uchaguzi Mkuu wa 2027 utakuwa kipimo muhimu kwa Rais William Ruto ambapo kwa mara ya kwanza tangu 2002 Raila Odinga hatakuwa katika ramani ya siasa ya Kenya.
Raial Odinga alikufa akiwa na miaka 80 / Reuters
24 Desemba 2025

Mwaka 2025, Kenya ilipoteza Waziri Mkuu wake mstaafu Raila Oding akiwa na umri wa miaka 80.

Maishani, Raila Amolo Odinga alitambulika kama mtetezi wa demokrasia ambaye mara kwa mara alibadilisha hali ya kisiasa ya Kenya kupitia ushirikiano wake wa kimkakati na viongozi tofauti.

Jukumu la ‘kupeana mikono’ alilofanya na marais wanne wa Kenya kwa lengo la kuzima vurugu na kuleta hali ya utulivu wakati wa mivutano katika nyakati tofauti baada ya uchaguzi.

Baada ya kifo chake, ndani ya chama chake, Orange Democratic Movement (ODM) tayari msukosuko umeanza kushuhudiwa, huku kukiwa na mgawanyiko kuhusu iwapo wataunga mkono azma ya Rais William Ruto kuchaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Raila aliwahi kufanya makubaliano na Rais William Ruto ambayo yaliwafanya baadhi ya wanachama kutoka chama chake kupata nyadhifa za juu serikalini chini ya 'mpango wa serikali jumuishi' au 'broad based government.'

Lakini pengine swali la Kenya baada ya Odinga ni iwapo kizazi kijacho cha viongozi wa kisiasa, chini ya shinikizo linaloongezeka la wananchi, wanaweza kuona jinsi matamanio yao binafsi yanavyoweza kutimizwa kwa kuitikia matakwa ya wananchi, na si uwezo wao wa kuleta pamoja miungano na mikataba baina yao.

Wataalamu wa masuala ya kisiasa wanasema uchaguzi wa 2027 utakuwa mtihani muhimu.

Huenda Rais Ruto akakabiliwa na changamoto ya kujaribu kuwashawishi Wakenya kwamba anashikilia ahadi alizowaahidi lakini hakuna Rais Kenya aliyewahi kuondoka madarakani kutokana na kushindwa katika uchaguzi. Haijulikani mpinzani wake mkuu atakuwa nani, kwa sababu kwa mara ya kwanza tangu 2002, hatakuwa Raila Odinga.

Wataalamu wengine wanasema kizazi cha vijana maarufu, Gen Z, kimeleta mwelekeo mpya katika siasa.

Bila kutegemea kabila au wanasiasa maarufu, badala yake kudai utoaji wa huduma, wanaweza kusababisha siasa za Kenya kwenye msimamo uliokomaa zaidi.

Swali ni je, vijana hawa wa Kenya wataleta mshikamano na nguvu kwenye sanduku la kura kwa imani kwamba italeta mabadiliko?