Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema siku ya Ijumaa kuwa imepokea ripoti za takriban watu 10 kuuawa na maafisa wa usalama wakati wa maandamano kufuatia uchaguzi mkuu mapema wiki hii.
"Tunasikitishwa na vifo na majeruhi yaliyotokea katika maandamano yanayohusiana na uchaguzi yanayoendelea nchini Tanzania,” msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Seif Magango aliwaambia waandishi mjini Geneva, akinukuu "vyanzo vya kuaminika" nchini humo.
“Ripoti ambazo tumepokea zinaonyesha kuwa watu wasiopungua 10 waliuawa," alisema.
Maandamano yalizuka katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine wakati wa upigaji kura siku ya Jumatano kupinga kutengwa kwa wapinzani wawili wakuu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kinyang'anyiro cha urais, pamoja na kile waandamanaji wanasema ni kuongezeka kwa ukandamizaji kutoka kwa serikali.
Serikali ya Tanzania imesema kuwa hali itarejea kuwa tulivu hivi karibuni.









