Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameonesha wasiwasi mkubwa kufuatia kuongezeka kwa ghasia nchini Sudan Kusini, akisema kuwa mapigano mapya yanazidisha hali mbaya ya kibinadamu na kusababisha wimbi kubwa la raia kuhama makazi yao.
“Katibu Mkuu ana wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa kuongezeka kwa ghasia nchini Sudan Kusini, hivi karibuni katika jimbo la Jonglei, ambazo zimesababisha vifo vingi, majeraha na raia 180,000 wanaripotiwa kuhama makwao,” amesema msemaji wake Stephane Dujarric katika taarifa.
“Katibu Mkuu pia ana wasiwasi mkubwa kuhusu athari za kuongezeka kwa ghasia kwenye mazingira ambayo tayari hali ya kibinadamu ni mbaya,” aliongeza, huku akiinukuu ripoti ya serikali ya Sudan Kusini inayosema kwamba takriban raia 250,000 walihama makazi yao katika wiki za mwanzo za 2026.
Akitaka serikali ya Sudan Kusini na vikosi vya upinzani 'kuchukua hatua za haraka na thabiti kusitisha operesheni zote za kijeshi,' Guterres aliwasihi 'kupunguza mzozo kupitia mazungumzo jumuishi.'
'Suluhisho la kisiasa'
“Katibu Mkuu anasisitiza kwamba mgogoro nchini Sudan Kusini unahitaji suluhisho la kisiasa, si la kijeshi,” taarifa hiyo ilisema, ikizitaka pande zote kukubaliana juu ya 'mpango wa hatua inayotegemea makubaliano kwa mwaka wa mwisho wa kipindi cha mpito ili kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi wenye uhalali.”
“Aidha anakaribisha juhudi zinazoendelea za Umoja wa Afrika na IGAD (Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo) na anazihimiza nchi jirani kuongeza msaada wao kwa ajili ya mazungumzo jumuishi,” iliongeza.
Sudan Kusini, nchi changa zaidi duniani, ilipata uhuru Julai 2011 lakini ikaingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir Mayardit kumfuta kazi Naibu wake wa Rais wakati huo, Riek Machar, akidai alikuwa akipanga mapinduzi.
Licha ya makubaliano ya amani ya 2018 na kuundwa kwa serikali ya umoja ya mpito, mapigano na mvutano wa kisiasa umeendelea.
Mvutano
Mapigano kati ya SSPDF na Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan - Upinzani (SPLA-IO), linaloongozwa na Oyet Nathaniel, makamu mwenyekiti wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan - Upinzani (SPLM-IO), yamezidi kuongezeka tangu Disemba katika kaskazini mwa Jonglei.
Mvutano uliongezeka mwanzoni mwa 2025, ukaonesha mgawanyiko ndani ya serikali ya mpito iliyoanzishwa chini ya makubaliano ya amani ya 2018. Mapigano yaliripotiwa kwa mara ya kwanza Januari katika Jimbo la Equatoria Magharibi kabla ya kuenea kaskazini.
Naibu wa Kwanza wa Rais Riek Machar amewekwa chini ya kifungo nyumbani tangu Machi 2025 na anakabiliwa na kesi mahakamani.

















