Kwanini kuanguka mtihani sio kuanguka maisha
AFRIKA
4 dk kusoma
Kwanini kuanguka mtihani sio kuanguka maishaKutopata daraja halisi ulilotaka au kukosa nafasi ya kuingia Chuo Kikuu haimaanishi kuwa maisha yako ya baadaye yamefungwa.
Kenya yafungua milango yake ya taasisi za masomo y ajuu kwa wanafunzi waliopata D/ Picha KNEC / others
20 Januari 2026

Collins Odhiambo ni mfanyakazi wa huduma za kijamii nchini Sudan Kusini. Kwa miaka mingi amekuwa akifanya kazi hii katika nafasi mbalimbali; akianzia kama mhudumu wa kujitolea na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Wakati alipokuwa shuleni, Collins alikuwa na ndoto kusomea ualimu. Hata hivyo, ndoto hiyo haikutimia baada ya kukosa kupata alama zilizohitajika kwenye mtihani wake wa sekondari.

‘‘Sikupata alama zilizohitajika kwenye mtihani wangu wa mwisho. Nilipata D,’’ anasema Collins katika mahojiano yake na TRT Afrika. ‘‘ Nilitaka kuwa mwalimu tangu zamani, lakini kila nikiomba nafasi nilikuwa na pata jibu la kuvunja moyo,’’ anakumbuka Collins.

Kwa wanafunzi wengi, mitihani ya kumaliza shule ya upili kama vile KCSE (Cheti cha Kenya cha Elimu ya Sekondari) huhisi kama maamuzi ya mustakabali wako. Lakini kama alivyogundua Collins, alama kwenye mitihani, ni sehemu moja tu ya safari, na kutopata alama ulizotarajia sio mwisho wa ndoto zako.

Idadi ndogo ya wanafunzi kufikisha alama za vyuo

‘‘Kwa zaidi ya miaka miwili baada ya kumaliza sekondari, sikujua la kufanya. Nisingeweza kujiunga chuoni kuendelea na masomo yangu. Ilinibidi kufanya kazi mbalimbali za kujitolea hasa katika mashirika yasiyo ya serikali, na hapo ndipo nikapenda zaidi huduma ya jamii na nikafuatilia zaidi,’’ anaeleza.

Kila mwaka, mamia ya maelfu ya wanafunzi hufanya mtihani wa sekondari KCSE. Hata hivyo, ni sehemu ndogo tu inayofikia daraja la chini (C+), ambalo ni kigezo cha kuingia moja kwa moja katika programu za shahada ya kwanza katika vyuo vikuu vya umma na vya kibinafsi.

Wanafunzi wapatao 965,000 nchini Kenya, walifanya mtihani wa KCSE mwaka 2024. Kati ya hao, ni wanafunzi 244,563 tu, waliobahatika kupata alama ya C+ na zaidi, kiwango cha chini cha kawaida kwa programu za shahada za kwanza.

Hata miongoni mwa waliohitimu, makumi kwa maelfu hawakutuma maombi ya kupangiwa nafasi katika Vyuo Vikuu kupitia mfumo mkuu wa upangaji vyuoni (KUCCPS), huku baadhi ya waliotuma maombi, wakikosa nafasi kutokana na idadi kubwa ya maombi.

Wanafunzi wapewa fursa zaidi

Kwa jumla, KUCCPS ilifanikiwa kudahili wanafunzi wapatao 310,000 katika Vyuo Vikuu na taasisi nyinginezo za elimu ya juu nchini Kenya, kwa ajili ya kozi mbalimbali, kama vile cheti, shahada za kwanza na astashahada.

Kenya inafanya jitihada kudahili wanafunzi zaidi kuendelea na masomo yao kwa ajili ya taaluma za baadaye.

Mwaka huu, taasisi ya KUCCPS inayowapanga wanafunzi vyuoni, imetangaza kushusha alama za wanafunzi watakaopewa nafasi katika chuo cha masomo ya afya KMTC, hadi D.

Hii itawapa wanafunzi wengi zaidi fursa katika fani hiyo.

Kozi zinagawanywa kwa vyeti na stashahada

Chini ya mpango huu wanafunzi wataanzia ngazi ya vyeti, stashahada, na hutolewa katika taasisi mbalimbali za mafunzo ya matibabu nchini kote.

Katika kiwango cha cheti, kozi zinazopatikana ni pamoja na Msaidizi wa Afya ya Jamii, Usimamizi wa Bima ya Afya, Rekodi za Afya na Teknolojia ya Habari.

Nyingine ni pamoja na Mtaalamu wa Ufundi wa Dharura wa Matibabu, Uhandisi wa Matibabu, Taaluma ya Lishe, Tiba ya Mifupa na Afya ya Umma.

Kozi za stashahada zinakuwa za taaluma ya juu zaidi kama Tiba ya Kliniki na Upasuaji, Afya ya Jamii, Afya ya Kinywa na Teknolojia ya Meno na nyinginezo.

Collins anashauri vijana waliokosa alama za kusajiliwa vyuo, wasikate tamaa, bali wazitolee macho fursa nyinginezo mbadala, ambazo ana uhakika kuwa zitawajenga na kuwafikisha watakapo.

Ushauri nasaha

‘‘Nilijaribu vitu vingi ikiwemo kufanya michezo ya kuigiza ya vitabu vya fasihi vya shule, nilifanya pia shughuli nyingi za kujitolea katika jamii, nikisaidia mashirika yasiyo ya kiserikali, kutokana na uzoefu wangu wa mitaa yetu na vijana wa mtaa. Hapo ndipo nilikuza uzoefu wangu na kutambua vyema taaluma nitakayofuatilia,’’ anaambia TRT Afrika.

Baada ya takriban miaka kumi na mbili, tangu amalize elimu yake ya sekondari, Collins alifanikiwa kujiunga na elimu ya ngazi ya Chuo Kikuu, ambapo anachukua shahada yake ya kwanza ya Sayansi ya Jamii na Maendeleo, kulingana na kazi anayofanya sasa na shirika moja lisilo la kiserikali.

‘‘Kutopata alama unayotaka haimaanishi kuwa umeshindwa-inamaanisha kuwa unaweza kuchukua njia tofauti kuelekea mafanikio. Njia hizi zinaweza kuwa za kuridhisha vile vile, ikiwa sivyo zaidi, kulingana na mambo yanayokuvutia na malengo yako.’’ anashauri Collins.

Mwaka 2025, takriban wanafunzi milioni moja walifanya mtihani wa kidato cha nne nchini Kenya. Kati yao , wanafunzi 1932 ndio waliopata alama ya A. Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu nchini Kenya, wanafunzi 270,000 pekee ndio waliofikisha alama C+ na zaidi kuingia Vyuo Vikuu.

Collins ana matumaini ya kumaliza elimu ya Chuo Kikuu akiwa na shahada yake, itakapofika mwezi Agosti 2026.

Japo hakuishia kuwa mwalimu kama ilivyokuwa ndoto yake ya mwanzo, Collins anaamini kuwa, safari yake itakuwa dira muhimu kwa wengine wengi waliokosa alama walizotaka.

CHANZO:TRT Afrika Swahili